Na Denis Chambi, Tanga.
HABARI njema kwa wadau wa mpira wa miguu Tanzania hususani mkoa wa Tanga ni kuwa kuanzia msimu ujao uwanja wa Mkwakwani utatumika kwenye mechi za kimataifa na hii ni baada ya wamiliki wa uwanja huo chama cha Mapinduzi 'CCM' kwa kushirikiana na shirikisho la Soka Tanzania 'TFF' kuamua kuufanyia maboresho ili kukidhi vigezo vya CAF.
Maboresho ya uwanja huo yamechochewa zaidi na klabu ya Coastal Union ambayo itashiriki kombe la shirikisho barani Afrika msimu ujao hivyo kuifanya Tanzania kuwa na viwanja vinne mpaka sasa vinavyokidhi kutumika kwa mashindano hayo makubwa barani Afrika ambavyo ni uwanja wa Amani uliopota Zanzibar, uwanja wa Benjamini Mkapa pamoja na uwanja wa Azam Complex ambao hutumika kwa hatua za awali pekee.
Akizungumza na vyombo vya habari Rais wa shirikisho la mpira wa miguu Tanzania 'TFF' Wales Karia amesema maboresho hayo yatakayofanyika ni katika sehemu ya vyumba vya kuvalia, sehemu ya waandishi wa habari, vyoo na maeneo mengine ikiwemo sehemu ya kuchezea 'Pitch' ambayo tayari nyasi zilizopo na udongo vimeshaanza kutolewa.
"Kuna upande wa jukwaa kuu, vyumba vya kubadilishia nguo, vyumba vya wanahabari , vyoo na vitu mbalimbali ambavyo vilitakiwa viwepo lakini jambo la haraka sana tuliona tuanze na sehemu ya kuchezea ambapo kuna mimea ambayo itapadwa aina ya Bamuda na kwa hali ya hewa ya Tanga ni kama Dar es salaam na tayari majani hayo yako njiani Sasa hivi ni maandalizi ya kuondoa majani na udongo uliopo ambapo tayari mchoraji ameshafika na kufanya tathmini".
"Suala la vyumba na jukwaa kuu tulishafanya utaratibu wa kumleta mchoraji na mpaka jumamosi hii tutapata michoro hiyo ya kuweza kurekebisha na kama tukifanikiwa tunatarajia uwanja wote tuweke viti vya kukalia mashabiki ili Coastal ikiingia hatua ya makundi mechi ziendelee kuchezwa hapa kwahiyo uwanja wa Mkwakwani utakuwa kwenye ngazi ya tatu kwa vigezo vya Caf"
Karia alisema maboresho hayo yatafanyika ndani ya miezi miwili na hadi kufika Augost 16, 2024 timu ya Coastal Union itaaza kucheza mchezo wake wa kwanza ikianzia nyumbani kwenye hatua za mtoano akiahidi kupeleka mashindano mbalimbali yenye hadhi ya kimataifa katika uwanja huo ikiwemo ya CECAFA ambayo yanatarajiwa kufanyika November 2024 .
"Marekebisho ya uwanja hayatachukua muda mrefu na kuna uwezekano mkubwa Augost 16 mechi ya nyumbani ya Coastal ikachezwa katika uwanja huu tunategemea marekebisho haya katikati ya mwezi July 2024 yatakuwa yameshaisha, sitakuwa na kigugumizi kuleta mashindano makubwa kwenye uwanja huu" aliongeza.
Mwenyekiti wa chama cha Mapinduzi 'CCM' mkoa wa Tanga Rajab Abdulrahmani alisema mara baada ya Coastal Union kukata tiketi ya kucheza kimataifa msimu ujao viongozi wa chama na Serikali waliona ni vyema kuweka mikakati ya kuboresha uwanja huo ili uweze kukidhi vigezo vya CAF na kuwezesha mechi zake zote zichezwe ndani ya CCM Mkwakwani.
"Katika siku kadhaa zilizopita tulileta Jenereta mpya ili kuruhusu na kuwezesha michezo ifanyike usiku na tuliahidi kuzishika mkono timu zetu za Coastal Union na African Sports, kama wana Tanga tukasema tushirikiane viongozi wa chama na Serikali ili kuhakikisha mashindano ya kimataifa yatakapoanza Coastal iutumie uwanja huu na sio vinginevyo" alisema Rajab.
Makamu mwenyekiti wa klabu ya Coastal Union Hassani Muhusini alisema baada ya kujihakikishia nafasi ya kushiriki kombe la shirikisho barani Afrika walitakiwa kutumia uwanja wa Amani uliopota Zanzibar kama uwanja wa nyumbani ambao ndio unaokidhi vigezo baadaye wakaona ipo haja ya kukaa na viongozi ili kuona uwezekano wa kurekebisha uwanja wa Mkwakwani iliwaweze kuitumia.
"Mafanikio ambayo Coastal Union imeyapata msimu huu ni ushirikiano uliokuwepo baina ya viongozi wa timu, chama na Serikali ya mkoa wa Tanga ,nia yetu ilikuwa ni vyema mechi zetu za kimataifa zifanyike hapa tunashukuru viongozi walipokea ombi letu na wanalitekeleza niwaombe sana wadau wa mkoa wa Tanga kutushika mkono ili kutimiza hili"
Post A Comment: