Tanzania inakuwa mwenyeji wa Mkutano wa 42 wa Baraza la Utawala la Umoja wa Posta Afrika (PAPU) linalotarajiwa kuanza Juni 3 hadi 14 , 2024 jijini Arusha yalipo Makao Makuu ya Ofisi za PAPU. Mkutano huo wa wataalamu utahudhuriwa na wajumbe kutoka nchi wanachama wa PAPU pamoja na wadau mbalimbali wa sekta ya posta kutoka barani Afrika na Umoja wa Posta Duniani.
Baraza la Utawala la Umoja wa Posta Afrika ni jukwaa muhimu kwa maendeleo ya sekta ya Posta barani Afrika ambapo viongozi wa posta kutoka nchi 46 wanachama watakutana kubadilishana uzoefu, kujadili changamoto na kutafuta suluhisho endelevu kwa ajili ya kuboresha huduma za posta katika mataifa yao.
Mkutano huu umegawanyika katika sehemu tatu ambapo kuanzia tarehe 3 -7 Juni, 2024 kutakuwa na vikao vya wataalamu wa masuala ya posta kutoka nchi mbalimbali za Afrika utakaofunguliwa na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar, Dkt. Mzee Suleiman Mndewa.
Tarehe 10 Juni, 2024 kutakuwa na Jukwaa la Wakurugenzi Wakuu wa Posta na Taasisi za Udhibiti wa Mawasiliano (CEOs Forum) watakaojadili na kupanga mipango ya maendeleo ya sekta ya posta barani Afrika na tarehe 11-12 Juni, 2024 kutakuwa na kikao cha Baraza la Utawala la PAPU. Tarehe 13-14 Juni, 2024 kutakuwa na Mkutano wa kujadili Mkakati wa Dunia wa Maendeleo ya Posta wa Mwaka 2025-2029, utakaowaleta wadau mbalimbali kutoka Afrika na Duniani.
Mkutano huu unafanyika nchini, baada ya Tanzania kuonyesha uongozi thabiti na dhamira ya dhati katika kukuza na kuimarisha huduma za posta na kutekeleza mfumo wa utambuzi wa Anwani za Makazi kwa asilimia 95. Hivyo, kwa kuandaa mkutano huu, Tanzania inatoa chachu na mchango mkubwa katika juhudi za kuboresha miundombinu na utoaji wa huduma za posta katika nchi za Afrika.
Mkutano huu utakuwa na mchango mkubwa na kuleta mabadiliko chanya katika sekta ya posta ambapo wajumbe wa Baraza hilo watakuwa na nafasi ya kujadili masuala muhimu kama vile ushirikiano wa kikanda, maendeleo ya kiteknolojia, na njia za kuboresha huduma za posta ili kukidhi mahitaji ya wateja wa kisasa.
Post A Comment: