Wagonjwa takribani 650 kutoka Mkoani Arusha wamehudumiwa ndani ya siku mbili kwa kupatiwa vipimo na matibabu kwenye banda la Taasisi ya Tiba ya mifupa Muhimbili (MOI) ikiwa ni taasisi pekee bobezi katika matibabu ya mifupa, ajali, upasuaji wa ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Takwimu hizo zimetolewa na Daktari Lemery Mchome, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya mifupa, upasuaji wa mishipa ya fahamu na Ubongo (MOI) wakati alipokuwa akizungumza na wanahabari kuhusu huduma wanazozitoa kwenye Kambi ya Matibabu ya madaktari bingwa inayoendelea kwenye Viwanja vya Sheikh Amri Abeid Jijini Arusha.

Dkt. Mchome pia ametumia nafasi hiyo kumshukuru kwa ushirikiano Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda kwa kuandaa kambi hiyo ya matibabu akisema Kambi hiyo inawasaidia kufahamu kuhusu huduma wanazozitoa pamoja na mahitaji yaliyopo kwenye Jamii.

Katika kambi hiyo Dkt. Lemery Mchome aliyeambatana na madaktari wengine bingwa kutoka kwenye Taasisi ya MOI amesema wanatumia Kambi hiyo pia kutoa elimu kwa wananchi wa Mikoa ya Kaskazini ili kuweza kujitambua afya zao na kujikinga dhidi ya hatari zenye kusababisha matatizo ya mifupa na  mishipa ya fahamu na ubongo akiahidi pia kuendelea kuwafutilia kwa ukaribu wagonjwa wote watakaobainika Mkoani Arusha.





Share To:

Post A Comment: