Naibu Waziri wa Madini Mhe. Dkt. Steven Kiruswa amekutana na kuzungumza na Naibu Waziri wa Nishati wa Nchini Marekani Mhe. David Turk katika kikao maalumu cha kujadili fursa zilizopo katika Sekta ya Madini hususan Madini Mkakati ambayo yanahitajika  sana kwa sasa Duniani huku Tanzania ikiwa imejaliwa aina mbalimbali za madini hayo.

Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika leo Juni 12, 2024 katika ukumbi wa ofisi ndogo ya Wizara ya Madini uliyopo Jijini Dar es Salaam, Dkt. Kiruswa ameupongeza ujumbe huo kwa kuchangamkia fursa za uwekezaji zilizopo nchini Tanzania na kuonesha nia ya kuwekeza nchini.

Aidha, Dkt. Kiruswa amesema Tanzania imebarikiwa kuwa na uwepo mkubwa wa madini mkakati lakini inakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa teknolojia katika maeneo mbalimbali ikiwemo eneo la utafiti, uchimbaji, uchenjuaji na uongezaji thamani wa madini hayo.

Katika hatua nyingine, Dkt. Kiruswa ameueleza ujumbe huo kuwa Tanzania ni sehemu salama ya uwekezaji ambapo nchi hiyo ina utulivu wa kisiasa, Sera na Sheria nzuri katika eneo la uwekezaji ambapo amewakaribisha wawekezaji kutoka Marekani kuwekeza nchini.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati wa nchini Marekani Mhe. David Turk ameishukuru Wizara ya Madini na Taasisi zake kwa makaribisho mazuri na kuonesha nia na utayari wa kushirikiana na nchi hiyo katika uwekezaji kwenye Sekta ya Madini hususan Madini Mkakati. 

Aidha, Waziri Turk amesema, matumizi ya Madini Mkakati ni muhimu Duniani kote kwa sababu yanazalisha nishati safi na kulinda mazingira ambapo pia amesema Marekani imeendelea katika maeneo mbalimbali ikiwemo eneo la teknolojia hususan katika eneo la utafiti, uchimbaji, uchenjuaji na uongezaji thamani madini.

Ujumbe wa Waziri Turk umeambatana na viongozi mbalimbali akiwemo Naibu Waziri anayeshughulika na masuala ya Ulaya, Asia na Afrika Josh Voly, Balozi wa Marekani nchini Tanzania Michael Battle na Wataalamu wengine.

Madini Mkakati ambayo kwa sasa Dunia inauhitaji mkubwa wa madini hayo yanayotumika katika teknolojia ya kisasa ikiwemo kutengenezea betri za magari ya umeme,  betri za simu, oil, grisi, break pad za magari, penseli na vizuia joto.

Baadhi ya Madini Mkakati yanayo patina nchini Tanzania ni pamoja na Kinywe, Nikeli, Lithiam, na Kobati.Share To:

Post A Comment: