Serikali imesema kuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kwa sasa inaendelea na hatua ya utafiti wa uanzishwaji wa matumizi ya Sarafu za Kidijitali za Benki Kuu (Central Bank Digital Currency) hapa nchini.

Hayo yameelezwa bungeni, jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), wakati akijibu swali la Mbunge wa Kigamboni, Mhe Dkt.Faustine Engelbert Ndugulile, aliyeuliza Serikali ina mpango gani wa kuanza kwa matumizi ya Sarafu za Kidijitali (Central Bank Digital Currency) hapa nchini. 

Mhe. Chande alisema kuwa Benki Kuu imebaini kwamba, kama ilivyo kwa mataifa mengi, uanzishwaji wa Sarafu za Kidijitali za Benki Kuu (Central Bank Digital Currency), unahitaji kuanzishwa kwa uangalifu na umakini bila kuleta athari hasi katika mifumo ya malipo iliyopo nchini na pia kuweza kutatua tatizo halisi la malipo ambapo kwa sasa bado mifumo iliyopo nchini inakidhi hali halisi ya uwezeshaji mwananchi kutuma fedha na kufanya malipo. 

‘‘Soko letu bado linahitaji kuendelea kuboreshwa katika kuimarisha mifumo iliyopo kwa kutumia vyanzo vinavyopatikana kwa urahisi na wananchi wengi (simu za kawaida) tofauti na matumizi ya Sarafu za Kidijitali zinazoitaji matumizi ya simu janja (smartphones),’’ alisema Mhe. Chande. 

Mhe. Chande alisema kuwa nchi nyingi ikiwa ni pamoja na majirani zetu na ukanda wetu bado wapo katika hatua hizi za awali za utafiti na kuboresha mifumo ya malipo iliyopo. 

Waziri wa Fedha Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), amesema kuwa Serikali inaendela na utafiti kuhusu matumizi ya fedha za kielektroniki kuangalia namna nchi inaweza kunufaika endapo itahamia kwenye matumizi ya fedha za mfumo huo wa kielektroniki. 

‘‘Utafiti unaendelea na sasa wanaangalia uzoefu katika mataifa ambayo yameanza kutumia fedha za kidigitali ikiwemo Nigeria na nchi za Asia na baada ya kukamilika hatua zitafuata kwa utaratibu unaofaa,’’ alifafanua Dkt. Nchemba.

Share To:

Post A Comment: