1000240250

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ameeleza kuwa Wizara ya Ujenzi imejipanga kuhakikisha inasimamia na kutekeleza maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kusimamia ujenzi wa miradi na ukarabati wa miundombinu ya barabara na madaraja nchini.

Ameeleza hayo Bungeni leo June 24, 2024 katika kikao na Wabunge Wanawake wenye Majimbo ambapo pamoja na mambo mengine amewapongeza Wabunge hao kwa kuwa na mkakati wa umoja na kujipanga vyema katika kuhakikisha wanaunga mkono juhudi zinazoendelea kufanywa na Serikali.

1000240282

“Waheshimiwa Wanawake huu ni muda wenu, nimefurahi kusikia mitazamo yenu mbalimbali ya kimkakati na niwahakikishie Wizara ipo pamoja nanyi na inatambua mtaji wa kinamama katika miradi mbalimbali ya ujenzi na matengenezo ya barabara na niwahakikishie tupo tayari kusimamia vyema maono ya Rais”, amesisitiza Bashungwa. 

Bashungwa ameeleza kuwa Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshaipa maelekezo Wizara ya Ujenzi na Wizara ya Fedha kukaa kwa pamoja kuangalia namna ya kupata fedha kwa ajili ya kuendelea kukamilisha miradi na kufanya matengenezo ya miundombinu ya barabara na madaraja yaliyoathiriwa na mvua za El-Nino.

Aidha, Bashungwa ameeleza Mkakati wa Serikali wa kuongeza bajeti ya Wizara ya Ujenzi ambapo Wizara ya Fedha imeshawasilisha Bungeni mapendekezo ya vyanzo vitatu vya mapato kwa ajili ya kuongeza Mfuko wa Barabara na kusisitiza kuwa mapendekezo hayo yakipitishwa na Bunge yatasaidia kuongeza fedha za matengenezo kwa ajili ya kuhudumia barabara za Mikoa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Wabunge Wanawake ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Same Mashariki, Mhe. Anna Malecela ameishukuru Wizara ya Ujenzi kwa kukutana na Wabunge Wanawake wenye majimbo na kuweka mikakati ya kusimamia utekelezaji wa maombi yaliyowasilishwa na Wabunge hao.

Naye, Mbunge wa Jimbo la Mchinga, Mhe. Salma Kikwete amemsisitiza Waziri Bashungwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi kujikita katika utekelezaji na utatuzi wa changamoto zilizowasilishwa na umoja huo kwa ajili ya maslahi ya wananchi na Taifa kwa ujumla.
1000240254
1000240278
1000240274
1000240266
1000240262
1000240270
Share To:

Post A Comment: