Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda usiku wa Ijumaa Juni 08, 2024 amewasihi Waongoza watalii wa Mkoa wa Arusha kuwa waadilifu, wenye lugha nzuri na vinara wa kuutangaza vyema Ukarimu wa Watanzania kwa kila Mgeni na Mtalii watakaebahatika kumuhudumia ndani ya Mkoa wa Arusha.
Mhe. Mkuu wa Mkoa ametoa kauli hiyo wakati akihutubia kwenye ufunguzi wa msimu wa tisa wa programu ya "Safari Field Challenge" yenye lengo la kumpata Mwongoza watalii bora wa mwaka, Shughuli iliyofanyika kwenye ukumbi wa Grand Melia Jijini Arusha ikiongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Hassan Abbas aliyemuwakilisha Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Angellah Kairuki.
Katika hotuba yake Mhe. Paul Makonda amewapongeza waongoza watalii hao kwa kazi nzuri akiwasisitiza kuwa wao ndiyo mabalozi wakuu wa kudhihirisha kwa vitendo kauli za Rais Samia Suluhu Hassan alizozitoa wakati wa filamu ya The Royal Tour pamoja na mahojiano mbalimbali kwenye vyombo vya habari vya kimataifa na kwenye mijadala kadhaa ambapo amekuwa akisisitiza juu ya ukarimu wa Watanzania na vivutio vya utalii vilivyopo nchini.
Mkuu wa Mkoa pia amewashukuru Waongoza watalii hao kwa ushirikiano mkubwa waliompatia tangu kuteuliwa kwake kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, akikumbusha zaidi ushirikiano wao wakati wa Ziara yake ya Siku sita za kutembelea Halmashauri zote za zilizopo mkoani Arusha iliyotamatika hivi karibuni.
"Tunawapongeza sana Waziri Kairuki na Dkt Abbas kwa kuendelea kuwa chachu na msukumo mzuri ambao umetiririka mpaka chini kwa watu wa Tanapa, Ngorongoro na hatimae wote wanaona thamani ya ndugu zetu hawa (Waongoza watalii), wanaofanya kazi kubwa ambayo labda mwingine angeweza kusema huyu si dereva tu, mtu wa kusema tu hapa kuna mnyama au hapa kuna matope, lakini tumekutana usiku huu kujadili kazi zenu. Nawapongeza sana" Ameongeza Mhe. Makonda.
Katika hatua nyingine pia Mhe. Makonda amewataka wana Arusha kutumia vyema fursa za Utalii zinazojitokeza Mkoani hapa na kueleza kuwa Tanzania ni nchi tajiri hivyo tumshike mkono Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na kuyaelewa maono mema aliyonayo kwa kila Mtanzania.
Mkuu wa Mkoa pia ametumia fursa hiyo kueleza namna ambavyo Arusha imebahatika kuwa na mfululizo wa matukio mbalimbali wakati huu, na kusema yapo matukio yatakayofanyika kwa mwaka huu mzima ikiwemo maonesho ya magari, tukio la Wanyamapori Festival pamoja na Tamasha kubwa la maharusi litakalofanyika baadae mwaka huu.
Mkuu wa Mkoa Mhe. Paul Christian Makonda kadhalika amewahakikishia wageni na watalii wote kuhusu Ulinzi na usalama wawapo Mkoani Arusha, akiliagiza Jeshi la Polisi kuendelea kufanya doria za mara kwa mara ili kubaini na kuzuia uhalifu na wahalifu kabla ya kuleta madhara kwenye Jamii ya Arusha na wageni wanaofika mkoani hapa kwa shughuli mbalimbali ikiwemo za kitalii pamoja na biashara.
Post A Comment: