Na Christina Thomas Dar es salaam


 Mtandao wa jinsia nchini Tanzania TGNP umewahimiza wanawake kushiriki pamoja na kugombea nafasi mbalimbali za uongozi hasa kwa kipindi hichi ambacho tunaelekea kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa lengo likiwa ni kuleta usawa na haki katika maamuzi kwenye jamii, kimaendeleo, kiuchumi na katika ustawi wa jamii kwa ujumla.


Hayo yamesemwa na Lilian Liundi ambaye ni Mkurugenzi wa Mtandao wa jinsia nchini Tanzania TGNP wakati akifungua mafunzo ya siku tatu ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari kuhusu masuala ya ukatili wa kijinsia jambo ambalo limekuwa likiumiza jamii pamoja na kudidimiza jitihada mbalimbali za kupambana na vitendo hivyo.


Bi Lilian amesema kuwa japo sheria inalazimisha uwepo wa wanawake katika ngazi ya maamuzi lakini bado ushiriki wao ni mdogo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo mila kandamizi na hofu miongoni mwao.'Sheria za serikali za mitaa inasema kwamba theruthi ya wajumbe wa halmashauri ya kijiji wanatakiwa kuwa wanawake lakini unakuta taarifa kama hizo wanawake wengi hawazifahamu, pia sheria hiyo inawataka wajumbne wawili kati ya sita wa kamati ya mtaa wawe wanawake, tunasema hivyo kwa sababu mara nyingi wanawake wamekuwa wakisukumwa kwenye viti maalumu' amesema Bi Lilian.


Pia ameongeza kuwa licha ya uwepo wa viti maalumu ambavyo ni kwa ajili ya wanawake bado kuna haja ya kuielimisha jamii hasa wanawake wakulima kushiriki kugombea nafasi nyingine za uongozi kutokana na kuwa na uwezo kuongoza.


Nafasi za Uongozi kwenye maeneo ya vijijini zimekuwa zikichukuliwa na wanaume kwa asilimia kubwa, hivyo Bi. Lilian amesema kuwa wakati huu wanawake wanatakiwa kuwekeza nguvu na kuona fursa ya kiuongozi kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa.'Muktadha tulionao sasa tunajiandaa na uchaguzi wa serikali za mtaa, kwa hiyo hawa wanawake wa vijijini tunafahamu kuwa wana nafasi kubwa sana za kushika nafasi za maamuzi katika uchaguzi huo' amesema Bi Lilian.


Pamoja na mambo mengine amewaomba waandishi wa habari kuona namna bora kuhamasisha wanawake wanashiriki kugombea nafasi za uongozi kwa kuwapa taarifa na habari sahihi kuhusu uongozi ili waweze kutumia nafasi hiyo kuleta mageuzi. Mafunzo yanahusisha wanahabari kutoka mikoa mitatu ya Manyara, Wilaya ya Babati na Mbulu, Morogoro ni Gairo na halmashauri ya wilaya ya Morogoro  na Kilimanjaro katika wilaya ya Mwanga pamoja  na  Same ambapo TGNP  na Pelum wanatekeleza mradi wa wanawake wa vijijini kuleta mabadiliko RWCC kwa ufadhili wa Serikali ya Canada ambao utawanufaisha wakulima takribani 5364



 

Share To:

ASHRACK

Post A Comment: