Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba, Bw. Isaya  Mbenje, amesema kuwa Serikali itaanza  kutumia vikao vyake  rasmi  kutoa elimu ya huduma ndogo za fedha ili kupunguza  migogoro inayoendelea nchini kuhusu mikopo na watu kuchukuliwa mali zao kwa kushindwa  kulipa mikopo.

Bw. Mbenje alitoa ahadi hiyo wakati alipokutana na Timu ya Wataalamu ya Wizara ya Fedha  ambayo ilifika Kisiwa cha Bumbire kutoa elimu ya fedha kwa Wananchi wa Kisiwa hicho ili waweze kujikomboa kiuchumi.

“Nitahakikisha Waratibu wa Elimu Ndogo ya Fedha ngazi ya Wilaya wanapata muda wa kutoa elimu katika vikao rasmi vya Serikali ambavyo vinawahusisha watu wengi wakiwemo Waheshimwa Madiwani na watu wote ili waweze kufikisha elimu hii kwa watu wanaowasimamia”, alisema Bw. Mbenje.

Alisema  kupitia Waheshimiwa Madiwani ambao ni Wawakilishi wa Wananchi katika ngazi ya Kata na Vijiji wakipewa elimu ya fedha vizuri na kuelewa itawafikia wananchi wengi katika maeneo yote kwa kuwa kila Kata na Vijijini inawawakilishi katika mikutano rasmi ya Serikali.

Kwa upande wake Afisa Mtendaji wa Kata wa Kisiwa cha Bumbire, Bw. Davis Alistedius, alisema kuwa kupitia elimu waliyoipata wananchi wa Kisiwa chake watahakikisha wanawasimamia waweze kusajili biashara zao ili ziweze kutambulika rasmi na Serikali ili kuwawezesha kufanya kazi kwa uhuru.

Naye mkazi wa Kisiwa cha Bumbire, Bw. Anorld Rweyemamu, aliishukuru Serikali kupitia Wizara ya Fedha kuwafikia na kuwapa elimu hiyo muhimu itakayowakomboa kiuchumi kupitia mada mbalimbali walizofundishwa ikiwemo uwekezaji, mikopo na umuhimu wa kuweka akiba.

“Elimu tuliyoipata ni nzuri ila tunaiomba Serikali iendelee kuwashawishi wawekezaji hususan Taasisi za Fedha kama benki kuja kuwekeza katika Kisiwa chetu ili kupitia Taasisi hizo tuweze kujiwekea akiba na kufanya uwekezaji kupitia ununuzi wa hisa”, alisema Bw. Rweyemamu.

Naye Afisa Usimamizi wa Fedha Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha Wizara ya Fedha, Bi. Mary Mihigo, aliwashukuru Wananchi wa Kisiwa cha Bumbire kwa kujitokeza kwa wingi kupata elimu ya fedha ambayo itawasaidia kuwa na matumizi sahihi ya fedha kutokana na mada mbalimbali walizowafundisha ikiwemo usimamizi wa fedha binafsi. 

Wizara ya Fedha inaendelea na zoezi la  kutoa elimu ya fedha kwa wananchi wa makundi mbalimbali katika mikoa nane ikiwemo Kagera, Singida na Manyara ikiwa ni utekelezaji wa Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha kwa mwaka 2021/2022 hadi 2029/2030.






Share To:

Post A Comment: