Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda amesema Kelele na ukosoaji unaoelekezwa kwake na baadhi ya watu kutokana na Mtindo wake wa Uongozi zinampa ari na nguvu zaidi katika kuwatumikia wananchi wa Arusha.

Akizungumza na Maafisa na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi Wilayani Arumeru wakati wa kuanza ziara yake kwenye Wilaya hiyo leo Mei 28, 2024, Mhe. Makonda amesema kamwe hatoacha kuwafichua na kuwawajibisha wazembe, wabadhirifu na watendaji wavivu wanaokwamisha juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan katika kuwaletea wananchi maendeleo na kutaka aachiwe wakosoaji hao kwani anawamudu kikamilifu.

Mkuu wa Mkoa Mhe. Paul Christian Makonda ametoa kauli hiyo mara baada ya kupata salamu za pongezi kutoka kwa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Arumeru wakimtaka kutokurudi nyuma katika kuhakikisha ilani ya Chama na maelekezo ya Serikali ya awamu ya sita yanatekelezwa kikamilifu na wasaidizi wake ngazi ya Mkoa.

Akiwa Monduli Mkoani Arusha Jumatatu Mei 27,2024,Mkuu wa Mkoa alionesha kushangazwa na wakosoaji hao wanaodai kuwa anadhalilisha watumishi wenzake, akihoji wakosoaji hao walikuwa wapi mwanzoni mwa mwaka huu wakati Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan akidhalilishwa na baadhi ya watu kwenye mitandao ya kijamii.

Katika Hatua nyingine Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Arusha amekiomba Chama Cha Mapinduzi kuendelea kuwa jicho la kubaini na kueleza kuhusu kukwama kwa miradi mbalimbali na kuwataja kwa majina watendaji vikwazo wanaozembea katika kuwatumikia wananchi na kutekeleza ilani ya Chama hicho tawala nchini Tanzania.

Aidha Mhe. Makonda amesema Mkoa wa Arusha unapaswa kuondokana na malumbano ya kisiasa na badala yake wawekeze kwenye uchumi kwa kuhakikisha kila mwananchi ananufaika na fursa na mazingira mazuri ya kibiashara na uwekezaji yaliyowekwa na serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Arusha ameingia kwenye wilaya ya nne miongoni mwa wilaya sita za Mkoa wa Arusha ikiwa ni muendelezo wa ziara yake ya "Siku sita za moto" na amebainisha kuwa ataendelea kushughulika vilivyo na wazembe, wavivu na watendaji wenye kuendekeza vitendo vya rushwa na kuzalisha migogoro na kero mbalimbali.







Share To:

Post A Comment: