Kufuatia Wizara ya Kilimo kutangaza katika kuendelea na mkakati wa kuendelea na zoezi za usambazaji wa mbolea ya ruzuku nchini katika mwaka 2024/2025, Mkuu wa mkoa wa Njombe, Mhe. Anthony Mtaka ameipongeza Wizara hiyo kwa hatua zake za madhubuti za kuhakikisha Wananchi wa Mkoa wa Njombe wanaendelea kupata mbolea ya ruzuku ili kuongeza uzalishaji katika mashamba yao.

RC Mtaka amebainisha hayo wakati akizungumza katika kipindi cha Sentro kinachoruka Clouds TV ambapo amesema mkoa wa Njombe ni miongoni mwa mikoa yenye uzalishaji mkubwa nchini na akieleza kuwa hatua hizo za Wizara ya Kilimo ni shangwe kubwa kwa wakulima wa Njombe kwasababu wamejipanga kuwa na uzalishaji mkubwa kwenye mikoa ya Kusini.

"Upatikanaji wa ruzuku umekuwa chagizo kubwa kuhakikisha agenda ya kilimo kinaendelea katika ukanda huu" amesema RC Mtaka.

Akizungumzia uzalishajiwa viazi mviringo, Mhe. Mtaka amesema "Toka watu wameanza kupata unafuu wa kutumia mbolea, wakulima wameanza kuzalisha gunia 130 hadi gunia 200 za viazi kwenye ekari moja.

RC Mtaka ameongezea kuwa jitihada hizi za Serikali za utoaji wa mbolea ya ruzuku kwa wananchi umetoa hamasa kwa wakulima kuingia shambani na kuendelea na kilimo chenye tija.

Wizara ya Kilimo katika mwaka 2024/2025 itaendelea kutoa ruzuku ya mbolea na viuatilifu kupitia mpango wa ruzuku kwa mazao yote ambapo Serikali itaratibu uingizwaji wa tani 1,086,115 za mbolea na kuzisambaza kwa wakulima kwa mpango wa ruzuku utakaoendelea hadi mwaka 2025/2026 kwa lengo la kuimarisha usambazaji wa mbolea nchini.
Share To:

Post A Comment: