Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda ndani ya dakika zisizozidi kumi, amefanikisha malipo ya  Bwana Patric Swai ambaye ni msambazaji wa vifaa vya ujenzi kuweza kulipwa deni lake la Milioni 132 alilokuwa anaudai mfuko wa kunusuru kaya maskini TASAF mkoa wa Arusha.

Hayo yamefanikiwa wakati wa kufunga ziara ya kutembelea wilaya zote sita za mkoa wa Arusha ikifahamika kama siku sita za moto za Mhe. Makonda ambapo alikuwa akisikiliza na kutatua kero mbalimbali za wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya Kilombero Jijini Arusha.

Bw. Swai amemuambia Mkuu wa Mkoa kuwa deni lake hilo lina miaka mitatu sasa na amekuwa akilifuatilia kwa muda mrefu bila mafanikio kabla ya kuamua kufika kwa Mkuu wa Mkoa kumuomba aweze kumsaidia kulipwa deni lake.

Kulingana na maelezo, Bw. Swai amemueleza Mhe. Mkuu wa Mkoa kuwa alisambaza vifaa vya ujenzi kwenye kata za Olmoti, Olasiti na Elerai kwaajili ya ujenzi wa wa Jengo la utawala na madarasa, zahanati na Jengo la Wazazi na watoto huko Elerai kwa kuwapa Mchanga,Mawe na saruji.

Mkuu wa Mkoa Mhe. Makonda mara baada ya kumbananisha Mratibu wa TASAF wilaya ya Arusha walikubaliana kuwa Mkurugenzi wa Jiji Injinia Juma Hamsin amlipe Bw. Swai ndani ya siku tatu kwa mapato ya ndani ya Halmashauri kabla ya kuendelea na taratibu nyingine.

Share To:

Post A Comment: