Na Munir Shemweta, MLELE
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Mbunge wa Jimbo la Kauu Mhe, Geophrey Pinda ameitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kujenga mahusiano mazuri na wafanyabiashara wa eneo Majimoto katika halmasauri ya Mpimbwe wilaya ya Mlele mkoa wa Katavi.
Mhe, Pinda ametoa kauli hiyo tarehe 3 Mei 2024 wakati wa kikao cha pamoja kati ya Maafisa wa TRA Makao makuu na wafanyabiashara wa eneo la Majimoto kilichofanyika katika halmashauri ya Mpimbwe.
Kikao hicho cha siku moja kinafuatia kuwepo malalamiko kutoka kwa wafanyabiashara kuwa wamekuwa wakinyanyaswa na maafisa wa TRA katika eneo hilo jambo walilolieleza kuwa limekuwa likisababisha usumbufu katika biashara zao.
‘’Mimi kama mbunge wa jimbo la Kavuu niko tayari kutoa ushirikiano na TRA lakini ushirikiano huo uende sambamba na mamlaka hiyo kujenga mahusiano mazuri na wafanyabiashara ‘’ amesema Mhe, Pinda
Amesema, ni wajibu wake kuhakikisha maisha ya wafanyabiashara katika eneo la Majimoto yanakuwa rafiki na kusisitiza kuwa, eneo hilo linapoteza wateja wengi na sababu kuwa na mahusiano mabovu na walipa kodi.
Aidha, Mhe, Pinda amewataka maafisa wa TRA katika eneo hilo kutokuwa na dharau kwa wafanyabiashara na kuhoji unapomdharau mlipa kodi unategemea kitu gani huku akisisitiza mamlaka hiyo kutoa huduma nzuri kwa kwa wateja.
Kwa mujibu wa Mbunge huyo wa jimbo la Kavuu, Mamlaka ya Mapato Tanzania lazima maafisa wake wawe rafiki na wafanyabiashara ili kuondoa vikwazo vinavyoweza kupeleka mkwamo kwa wafanyabiashara.
Amebainisha kuwa, TRA pamoja na mambo mengine lazima ijikite kutoa elimu kwa mlipa kodi kama ambavyo maafisa wake walivyofanya kwa kwenda kwa wafanyabiashara wa Majimoto huku akiwataka maafisa hao kuacha kabisa siasa katika shughuli za kibiashara. ‘’Nasema haya ili mje na mageuzi makubwa kwa lengo la kuboresha’’. Amesema Mhe, Pinda
Kwa upande wake Mkurugenzi wa halmashauri ya Mpimbwe Bi. Shamim Daud amesema, zaidi ya asilimia hamsini ya mzunguko wa fedha katika halmashauri yake inatoka eneo la Majimoto na ndiyo maana halmashauri yake imeweka uwekezaji mkubwa katika eneo hilo ili kuhakikisha huduma za jamii zinaimarishwa na kupunguza changamoto kwa watu wanaoingia na kutoka eneo hilo.
‘’Kwa hiyo tunashukuru na tunatumaini kikao hiki watu watakapotoka watakuwa wamejifunza na TRA watakuwa wameelewa changamoto za maeneo hayo na kuwaletea mabadiliko makubwa’’. Amesema Mhe, Pinda.
Post A Comment: