FATUMA Kassim Hassani, askari magereza mstaafu, amepata ulemavu wa kudumu kutokana na ajali ya gari aliyoipata Machi, 2020, lakini hadi sasa ananyanyaswa na kampuni ya bima kupata fidia aliyostahili, Raia Mwema limebaini.
Askari huyo mstaafu aishie mkoani Tanga, ni miongoni mwa wananchi wanaohangaika kudai fidia kwenye kampuni za bima bila mafanikio huku kampuni hizo zikiwa zinaonyesha dharau na kujiamini kutochukuliwa hatua zozote.
Moja ya kampuni hizo ni Insuarance Group of Tanzania (IGT) ambayo Fatuma na wadai wengine wamekua wakisumbuliwa na kupata majibu yenye kukatisha tamaa au kudharauliwa pamoja na Mamlaka ya Udhibiti wa Bima Tanzania (TIRA) kuingilia kati.
Maofisa wa TIRA Kanda ya Kaskazini walioko mkoani Arusha, wameiandikia IGT barua mara kadhaa na kuwasiliana nao kwa njia mbalimbali lakini kampuni hiyo ya bima haijawahi kutoa majibu ikionyesha dharau na kiburi kilichopitiliza ikielezwa kuchagizwa na nguvu za wanasiasa.
Fatuma anayeidai IGT Shilingi 100, 404.800 zikiwemo Shilingi milioni 50 zinazotokana na majeraha (ulemavu wa kudumu), sasa anamlilia Rais Samia Suluhu Hassan kupitia viongozi wa mikoa ya Arusha ma Tanga ambako suala lake linashughulikiwa.
“Nimeomba msaada kwa Mkuu wa Mkoa wa Tanga mwanamke mwenzangu Dk. Batilda Buriani, na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda wanisaidie ili kupata haki yangu nikatibiwe India.
“ Nimefanyiwa operesheni 15 lakini bado vyuma havijakaa sawa napata maumivu makali. IGT hawataki kunilipa na wanachezea na kudharau hadi amri ya mahakama ya Tanga na amri ya TIRA Arusha, naomba wasaidizi wa Rais Samia wanisaidie nilipwe nikatibiwe,” anasema kwa uchungu Fatuma akiwa kitandani nyumbani kwake Tanga mjini.
“Hakuna jitihada zozote zilizofanywa na IGT kunilipa fidia, huku afya yangu ikizidi kuzorota na sehemu za maungio ya mwili zilizoathirika zaidi kiasi cha kuwekewa vyuma, kuzidi kupoteza uwezo wa kuhimili kunakosababishwa na kutopata matibabu kwa wakati, kwa vile sina fedha na IGT imeshindwa kutimiza takwa la kisheria kunilipa,” analalamika Fatuma.
Uchunguzi wa Raia Mwema umebaini kuwa kampuni hiyo ilianzishwa na Waziri mmoja Mstaafu, ambaye alikua na nguvu kubwa ya kisiasa na kiuchumi lakini pia kiburi na dharau kutoka kwa watendaji na wakurugenzi wenza wa IGT ambao wamekua wakiwadharau wadai.
Pamoja na Fatuma, wadai wengine wanaoidai kampuni hiyo wamediriki kufika katika ofisi za kampuni hiyo Mikocheni Dar es Salaam, bila mafanikio ya kupata haki zao za fidia.
Wakihojiwa na televisheni ya Azam ya UTV wadai wengine ni pamoja na Aisha Mweyane aliyesema kwamba aliahidiwa kulipwa zaidi ya Sh milioni 18 lakini amekuwa akizungushwa na kwamba mara ya mwisho aliahidiwa kulipwa shilingi mililioni 2.5 ila alijikuta akipewa shilingi laki 5 pekee Aprili 28, mwaka huu.
Naye Lyidia Vikavu alisema kampuni hiyo inasumbua kulipa waathirika lakini kwa upande wa wenye mabasi wanalipwa kwa wakati jambo ambalo linaonesha kuwa wanafanya makusudi kuwakwamisha.
“Kwa sababu ya kufuatilia madai yangu kwa miaka mitatu shughuli zangu zimesimama, lakini naumwa siwezi kujitibia kwani kila mara napaswa kuja hapa sio sawa kabisa,” alisema.
Aidan Chilubi alisema katika ufuatiliaji wa madai yao wamekuwa wakipigwa virungu na walinzi, wakichaniwa mashati pindi wanapotaka kuingia ndani kudai madai yao, hali ambayo inaonesha wahusika hawana nia njema.
Kwa upande wake Nurubani Mfinanga alisema hadi sasa hajalipwa kitu na kwamba wameahidiwa kulipwa kidogo kidogo na waliposema walipwe ndio waondoke walitakiwa kuondoka na kusubiria.
Ripoti ya Mkaguzi na Mdibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali ya miaka minne ilianisha kuwepo mrundukano wa madai ya bima ya shilingi bilioni 114.533 kwa mwaka 2019/20 na kupanda hadi shilingi bilioni 127.253 mwaka 2022/23 sawa na ongezeko la asilimia 11.
Katika ripoti hiyo CAG alisema ukaguzi wao kuhusu sekta ya bima walibaini uwepo ufanisi mdogo wa kushughulikia madai ya malipo ya bima, usimamizi mdogo wa utendaji wa taasisi za bima, uwezo mdogo wa kifedha wa kampuni za bima, kutozingatiwa kwa maoni ya wateja wa bima, na kutochukuliwa hatua kwa kampuni zenye ukwasi mdogo wa fedha,
CAG alisema pia changamoto nyingine waliyobaini ni elimu ndogo kwa umma kuhusu bima, kutokuwepo taarifa kuhusu maoni ya wateja, uelewa mdogo wa sera ya taifa ya bima, kupungua kwa wateja kutoka asilimia 15 mwaka 2017 hadi asilimia 10 mwaka 2023 na TIRA kuchagua baadhi ya kampuni kwa ajili ya ukaguzi.
Akijibu malalamiko hayo Meneja wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima (TIRA) Kanda ya Mashariki Muyenge Zakaria alisema kuhusu ulipaji wa madai kwao ni kipaumbele ambapo wanahakikisha makampuni yanalipa kwa wakati.
Kupitia televisheni ya UTV, Muyenge alisema makampuni ya bima yanalipa madai ya bima kwa asilimia 95 na asilimia 5 ndio ya malipo ndio imekuwa na changamoto ambazo zinasababishwa na wadai kukosa vielelezo.
“Kuhusu madai ni kipaumbele chetu TIRA na alisema mwaka 2019/20 madai yalikuwa shilingi bilioni 280 na shilingi bilioni 268 zililipwa ikiwa ni asilimia 4.2 ambao hawajalipwa, mwaka 2020/21 madai yalikuwa shilingi bilioni 315 na kampuni zililipa shilingi bilioni 301 sawa na asilimia 4 ndio haijalipwa. Sababu ya kutolipwa ni kukosekana vilelelezo,” alisema.
Alisema malalamiko ambayo yanatolewa yanatokana na asilimia 5 ya madai ambayo asilimia kubwa hawapeleki vielelezo, jambo ambalo linakwamisha ulipaji na kwamba walalamikaji ndio wamekuwa wakisikilizwa zaidi.
Zakaria alisema TIRA haiwezi kuvumilia kampuni ambayo inakwamisha ulipaji wa bima na kwamba wamekuwa wakichukua hatua kwa mujibu wa sheria.
Meneja huyo wa Kanda ya Mashariki alisema zipo kampuni zaidi ya 1,500 ambazo zinakaguliwa na kanda 10 zilizopo kila siku, hivyo ni ngumu kujua kuna mteja anadai na halipwi na kunyamaza.
“Suala la utoaji elimu sio la mamlaka ni la makampuni ya bima na wamekuwa wakitoa elimu bila changamoto yoyote na uzuri wateja wakikwama wanawasiliana na TIRA kwa uthibitisho.
Alisema Kamshina wa TIRA ameweza kutembelea kanda 10 na kukutana na zaidi ya wananchi 1,350, hivyo hata wao wanapambana kuhakikisha jamii inapata uelewa wa huduma za bima.
“Sisi mamlaka tunajukumu la kutoa elimu na mwaka huu wa fedha 2023/24 kamishna wa TIRA ameweza kutembelea kanda zote na kufikia zaidi ya wananchi 1,350,” alisema.
Post A Comment: