Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga Mhe. Ngassa Mboje akizungumza kwenye baraza la madiwani la Halmashauri hiyo leo katika kikao cha pili  mkutano wa robo ya tatu kwa Mwaka wa fedha 2023/2024.

Na Mapuli Kitina Misalaba

Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga leo Mei 10, 2024 limeridhia hoja ya kufukuzwa kazi mtumishi mmoja  kwa makosa mbalimbali ikiwemo utoro kazini zaidi ya muda wa siku tano (5).

Mtumishi huyo anaitwa  Msajigwa Julius Mwaipopo ambaye alikuwa idara ya Ugavi Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga na kwamba alikuwa anatuhumiwa kwa makosa mbalimbali ikiwemo utoro kazini.

Tamko la kufukuzwa kazi mtumishi huyo limetolewa kwa niaba ya madiwani na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga Mhe. Ngassa Mboje

Azimio hilo la Madiwani, limefanyika baada ya kuzingatiwa kwa taratibu zote za kisheria zinazotakiwa katika kuwawajibisha watumishi wa Halmashauri.

“Tulikuwa na shauri la kinidhamu moja leo la mtumishi mmoja na shauri hili kwa kauli moja baraza la madiwani nimemfukuza kazi mtumishi mmoja ambaye anatoka idara ya Ugavi jina anaitwa Msajigwa Mwaipopo kwahiyo haya yote tumeyafanya kwa pamoja niwashukuru sana wajumbe kwa sababu haya yote yamejikita kwenye sheria na taratibu zilizopo”.amesema Mhe. Ngassa Mboje

Wakati huo huo baraza la madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga limewathibitisha rasmi kazini jumla ya watumishi 51.

Aidha katika mkutano wa Baraza hilo Madiwani pamoja na viongozi wengine wamebainisha mambo mbalimbali ikiwemo changamoto za miundombinu pamoja na Maji huku taarifa mbalimbali zikiwasilishwa.

Katika taarifa yake  kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga Stewart Makali ameeleza kuwa ugonjwa wa kipindupindu umeipuka na kuua watu wawili kata ya Mwakitolyo.

Amesema Halmashauri hiyo ilipata wagonjwa 11 wa kipindupindu kati yao wawili wamefariki dunia na kusema jitihadi mbalimbali zinaendelea kuchukuliwa na wataalam wa Afya kwa kushirikiana na Halmashauri  ili kuthibiti ugonjwa huo.

“Halmashauri yetu imepokea taarifa za uwepo wa ugonjwa wa Kipindupindu ambapo tarehe 30.4.2024 jumla ya watu kumi na mmoja (11) waligundulika kuambukizwa ugonjwa huo katika kijiji cha Nyaligongo kata ya Mwakitolyo, watu wawili walifariki”.

“Wagonjwa tisa (9) waliobaki walipatiwa matibabu na kuruhusiwa na timu ya wataalam inaendelea kuwafuatilia, Halmashauri imeshachukua hatua za kukabiliana na ugonjwa huu kwa kugawa dawa za kutibu maji kwa kaya 462, kutibu visima vya maji 16, kutoa elimu ya jinsi ya kujikinga na maabukizi ya ugonjwa huu katika vitongoji vya namba moja, mbili na namba tatu”.

“Natoa wito kwa jamii yote kuendelea kuchukua tahadhari na kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huu kwa kuzingatia  kutumia choo kikamilifu, kunawa mikono kwa maji safi kabla na baada ya kufanya shughuli yoyote, usafi wa mazingira, kula chakula kikiwa cha moto pamoja na kunywa maji yanayotoka kwenye chanzo kinachoaminika na yawe yametibiwa”.amesema Makali

Misalaba Media  imezungumza na baadhi ya madiwani ambao wameipongeza Halmashauri hiyo kwa jitihadi inazozifanya huku wakisisitiza suala la usafi ili kuthibiti mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga.

Baraza la madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga leo limefanya kikao cha pili katika Mkutano wa robo ya tatu kwa Mwaka wa fedha 2023/2024.




 

Share To:

Misalaba

Post A Comment: