Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amesema Mheshimiwa Rais, Samia Suluhu Hassan ameilekeza Wiazara ya Ujenzi kuendelea kuboresha Mji wa Katesh wilayani Hanang na miundombinu ya barabara kutokana na Mji huo kuharibiwa na Maporomoko ya Matope yaliyotokea Disemba 2023.
Bashungwa ameyasema hayo Mkoani Manyara wakati akizungumza na wananchi na kueleza kuwa TANROADS itajenga tabaka la juu la lami katika barabara za mji wa Katesh zenye urefu wa kilometa mbili kwa ajili ya kurejesha miundombinu ya barabara iliyopata athari za maporomoko ya matope.
“Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan alituelekeza Wizara ya Ujenzi kuendelea kuweka mazingira mazuri katika mji wa Katesh kwa kurejesha upya miundombinu ya barabara iliyopata changamoto na Mkandarasi ameshapatikana”, amesema Bashungwa.
Aidha, Waziri Bashungwa ameeleza kuwa TANROADS watatengeneza mitaro ya mawe na zege na kujenga makalvati sita ili maji yanapokuwa yanapita yasiweze kuharibu miundombinu ambayo inajengwa kwa gharama kubwa.
“Ili kuendelea kuupendezesha mji wa katesh, tunaenda kujenga vivuko vya zege vya waenda kwa miguu ili kurudisha Miundombinu ya mji huo kama hapo awali ulivyokuwa,” amesema Waziri Bashungwa.
Kuhusu suala la taa za barabarani, Bashungwa ameeleza kuwa tayari TANROADS imeshanunua taa za barabarani kwa ajili ya kufungwa katika barabara kuu ili kupendesha mji wa Katesh.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga, amesema Mkoa wa Manyara ni moja ya mkoa uliobarikiwa kupata mvua nyingi na hivyo kusababisha barabara nyingi kuharibika lakini jitihada kubwa zinaendelea kufanywa na Wakala wa wa Barabara (TANROADS).
Post A Comment: