Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda ameagiza kupandishwa Mahakamani kwa watendaji wa Mkoa wa Arusha waliohusika na upotevu na wizi wa Milioni 428 zilizokuwa zimetengwa kwaajili ya mpango wa kunusuru kaya maskini TASAF.
Mbele ya wanahabari mjini Arusha, Mkuu wa mkoa Mhe. Paul Christian Makonda ametoa kauli hiyo mara baada ya kukamilika kwa uchunguzi uliokuwa ukifanywa na Taasisi ya kupambana na kuzuia Rushwa TAKUKURU mkoa wa Arusha.
Mhe. Mkuu wa mkoa ameiagiza TAKUKURU kufanya uchunguzi kwenye miradi yote saba ya mfuko wa TASAF mkoa wa Arusha ili kujiridhisha kuhusu thamani ya fedha iliyotumika kwenye miradi inayotekelezwa mkoani Arusha.
Katika hatua nyingine Mkuu wa mkoa Mhe. Paul Makonda ameonya kuhusu watendaji wabadhirifu na wanaoiba fedha za serikali na kusema hatofumbia macho mtu yeyote atakayeenda tofauti na miiko ya Utumishi wa Umma.
Mhe. Makonda ametangaza kuanza kwa uchunguzi maalum kuhusu matumizi ya fedha zinazotolewa na serikali kwaajili ya Utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo mkoani Arusha na kuahidi kuchukuliwa kwa hatua za kisheria kwa wote watakaobainika kujihusisha na wizi na matumizi mabaya ya fedha za maendeleo.
Post A Comment: