MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Ndg. Abdulrahman Kinana, amesema msaada mkubwa wa haraka unahitajika kwa wananchi walioathirika na mafuriko wilayani Rufiji, Mkoa wa Pwani.


Amesema hayo baada ya kupokea taarifa na kushuhudia hali ilivyo wilayani humo, ambapo kata 12 kati ya 13 zimeathirika, na kutaka serikali kuharakisha misaada kikiwemo chakula na malazi kwa zaidi ya watu 88,000 walioathirika.

Kinana ametoa wito huo leo, Aprili 9, 2024, alipokuwa akizungumza na wananchi wa vijiji vya Muhoro na Chumbi, baada ya kuwatembelea na kuwapa pole wananchi waliokumbwa na mafuriko hayo, yaliyotokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha na kusababisha Mto Rufiji kufurika katika makazi ya watu.

"Nimezungumza na Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa), kwa namna nilivyojionea na nimemweleza uharaka wa Mahitaji, sina shaka hata kidogo na yeye atakuja kujionea. Haraka ameitisha kikao na mawaziri wote wanaohusika na maswala ya maafa, nina hakika akishakuja hapa kasi ya kutoa huduma itaongezeka ” amesema.

Amesisitiza kuwa, kutokana na hali hiyo anaihimiza serikali kuongeza juhudi za kutoa huduma kwa wananchi waliopatwa na maafa hayo ambayo yameathiri pia shule na zahanati.

“Nimekuja kuwapa pole kwa niaba ya Rais, kwa niaba ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). Nimekuja kujionea hali ilivyo, lakini niendelee kutumia fursa hii kuihimiza serikali kuleta misaada haraka kwa wananchi walioathirika," amesisitiza Makamu Mwenyekiti Ndg. Kinana.Share To:

Post A Comment: