Na Stanley Mwalongo- MOI


Taasisi ya tiba ya mifupa na ubongo Muhimbili (MOI) kwa kushirikiana na Taasisi ya MO Dewji foundation imeandaa kambi  ya upasuaji kwa  watoto 50 wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi itakayofanyika tarehe 20/04/2024 katika taasisi ya MOI.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 8, 2024, Kaimu Mkurugenzi mtendaji  wa MOI Dkt. Lemeri Mchome amesema Taasisi ya MOI imejizatiti kuhakikisha watoto wengi wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi wanafikiwa na kupatiwa huduma ikiwemo na upasuaji bila gharama yoyote na kuwaomba  wazazi wenye watoto hao kufika  MOI aprili 13, 2024 kwaajili ya kliniki maalum, na wenye vigezo watafanyiwa upasuaji april 20, 2024.

“Lengo letu ni kuwafikia watoto wengi zaidi ambao hawajabahatika kupata matibabu kwahiyo tunashirikiana na Taasisi ya MO Dewji foundation kufanya  kambi hii  ya upasuaji kwa watoto 50 wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi” amesema Dkt. Mchome

Dkt. Mchome ameishukuru Taasisi ya MO Dewji foundation kuunga mkono jitihada za Serikali za kuhakikisha watoto wenye mahitaji maalum wanapata huduma bora za kibingwa na kibobezi bila gharama yoyote.

Naye, Mratibu wa mradi kutoka MO Dewji Bi. Amina Ramadhan amesema Taasisi hiyo itasaidia watoto hao 50 kabla na baada ya huduma ya upasuaji ikiwemo vipimo vitavyohitajika vya radiolojia, maabara na muendelezo wa matibabu kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Chama cha wazazi wa watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi (ASBATH) Bi. Suma Mwaipopo ameishukuru Taasisi ya MOI na MO Dewji foundation kwa ushirikiano wao wa kuwasidia watoto hao pia amewasihi wazazi kutoka mikoa yote wasikose kushiriki kambi hiyo.

Daktari wa ubongo wa MOI Dkt. Consolata Shayo amesema MOI imekuwa ikiwahudumia kwa ukaribu watoto hao wakiwa wodini, kwenye kliniki, vipimo na vyumba vya upasuaji hivyo amewaalika wote waliopo majumbani na mikoani waliowaficha watoto hao ndani waje kwa wingi siku ya kliniki tarehe 13/4/2024.

Meneja wa Ustawi wa jamii MOI, Jumaa Almasi amesema MOI ni Taasisi ya umma ipo kwaajili ya kuhakikisha watoto hao wanapata huduma hivyo wazazi wenye watoto hao wawasiliane na MOI kupitia no za simu zifuatazo: +255 767 296 992, +255 788 888 196. Kwaajili ya maelezo zaidi.







Share To:

Post A Comment: