KATIKA hali inayoonesha hamasa kuendelea kuwa kubwa kwa watu kutaka kuondoka kwa hiari ndani ya hifadhi ya Ngorongoro Jumla ya kaya 15 zenye watu 107 na mifugo 359 wa kabila la wamang’ati wameomba na hatimaye kuhamishwa kwa hiyari kuelekea katika Kijiji cha Msomera kilichopo wilayani Handeni Mkoani Tanga.
Kaya hizo ziliomba kuhama kwa hiyari kwa Kamishna wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na hivyo kuhamishwa katika hafla iliyofanyika siku ya Alhamisi ya tarehe 08.02.2024 katika ofisi za makao makuu ya zamani ya mamlaka hiyo.
Kamishna wa Uhifadhi Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro Bw.Richard Kiiza aliwapongeza wananchi hao kwa uamuzi wao huo wa kutaka kuondoka ndani ya hifadhi na kusema kuwa mamlaka imejipanga kuhakikisha mtu yoyote anayetaka kuhama kwa hiyari anahamishwa haraka iwezekanavyo.
“Kwa niaba ya serikali tunawapongeza sana,mmefanya kitendo cha ujasiri kwani huko mnakoelekea mtapata huduma zote muhimu ambazo zitafanya maisha yenu yawe bora na hivyo kuongeza tija katika na ustawi wa jamii yenu”ameongeza Kamishna Kiiza.
Wananchi hao wameipongeza serikali ya awamu ya sita inavyosimamia zoezi hilo ambapo wamesema wamefurahishwa na jinsi wanavyoondolewa ndani ya hifadhi kwa heshima kubwa na kusafirishwa wao na mifugo yao katika mazingira yanayozingatia utu wa binadamu.
Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kwa sasa imekuwa ikipokea maombi ya watu mbalimbali ya kutaka kuhama kwenye eneo hilo ambapo wananchi hao wamekuwa wakielekea katika Kijiji cha Msomera na hata maeneo mengine nchini.
Share To:

Post A Comment: