Makamu wa Rais, Mhe. Dkt. Phillip Mpango amewataka wananchi kutokata miti hovyo ili kulinda mazingira na uoto wa asili uliopo sasa.
Dkt. Mpango ameyasema hayo leo Februari 21,2024 katika kijiji cha Kabuku wilayani Handeni ikiwa ni siku ya kwanza ya Ziara yake ya Siku tatu mkoani Tanga.
Mhe. Dkt. Mpango amewataka wananchi kupanda miti kwa wingi ili kuhifadhi mazingira na kupambana na mabadiliko ya tabia Nchi ambayo kwa sasa yamepelekea kuwa na joto kali hasa kwa ukanda wa Pwani.
Vilevile, Mhe. Dkt Mpango alisisitiza jukumu la kutunza uoto wa asili ni la kila mtanzania hivyo ni vema kushiriki katika utunzaji wa mazingira kwa kupanda miti kwa wingi.
Awali akitolea ufafanuzi wa baadhi ya changamoto zilizotolewa na Mbunge wa Handeni Mjini Mhe. Kwagilwa Reuben Nhamanilo, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dunstan Kitandula(Mb) alimhakikishia Makamu wa Rais kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Angellah Kairuki(Mb) kuwa watazilinda maliasili za nchi hii kwa weledi na wivu mkubwa.
Mhe. Kitandula aliongeza kuwa wizara ya Maliasili na Utalii imefanya vikao na wabunge wa nchi nzima ikiwemo mkoa wa Tanga ili kusikiliza changamoto, ushauri na mapendekezo yao kuhusiana na sekta za wanyamapori, misitu, utalii na malikale.
Aidha,Mhe. Kitandula alisema kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii inatarajia kufungua Geti jipya la Kuingilia hifadhi ya Taifa ya Saadani kupitia eneo la kwa Msisi Wilaya ya Handeni mwaka ujao fedha 2024/2025.
Post A Comment: