SHIRIKA La Mawasiliano Tanzania (TTCL,) limeendelea kusambaza huduma nje ya mipaka ya Tanzania kwa kusaini hati ya makubaliano ya kibiashara yenye lengo la kuongeza huduma kwenye Mkongo wa mawasiliano na Mkongo wa Taifa wa Burundi (BBS.)

Akizungumza Leo jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya kusaini Mkataba huo Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye amesema mkataba huo mpya wa kibiashara wa miaka mitano wenye thamani ya Dola za Kimarekani Milioni 3.3/-(sawa na shilingi za kitanzania Bilioni 8.3/-) ni muendelezo wa uhusiano baina ya Nchi hizo mbili pamoja na juhudi za Serikali katika kuboresha sekta ya Mawasiliano.

“Serikali ya Awamu ya Sita kupitia TTCL imeonesha dhamira thabiti ya kusimamia sekta ya mawasiliano
nchini kwa kuweka mazingira bora ya uwekezaji, kukuza matumizi ya TEHAMA na huduma
za kidijitali, na kufungua fursa kwa nchi za Afrika Mashariki na SADC kutumia
miundombinu yetu ya mawasiliano kama vile Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano (NICTBB)
na Kituo cha Taifa cha Kuhifadhi Data Kimtandao (NIDC).” Amesema.

Nnauye ameishukuru Serikali ya Burundi na BBS kwa kuendelea kuiamini Tanzania na kutoa fursa ya kuwahudumia kupitia Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL,) ambalo limeendelea kuchanja mbuga kwa kutoa huduma nje ya mipaka ya Tanzania na kuahidi kuendelea kutoa huduma bora za Mkongo wa
Taifa wa Mawasiliano kwa lengo la kukuza maendeleo ya nchi hizo mbili pamoja na ukanda ya Afrika Mashariki.

“Ni kweli kabisa kwamba Jumuiya ya Afrika Mashariki inapaswa kuwa na mipango na mikakati ya kuendeleza sekta ya mawasiliano ndani ya Jumuiya, Kujenga mifumo ya kidijitali itakayowezesha Afya mtandao, Elimu mtandao, Biashara mtandao, Kilimo mtandao, Serikali ntandao, na malipo kwa kutumia mifumo ya kidijitali ambayo ni muhimu sana
katika kurahisisha shughuli za maendeleo kwa wananchi wetu.” Ameeleza Nnauye.

Aidha amesema kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan imeonesha dhamira thabiti ya kuwekeza katika miundombinu ya mawasiliano ya kimkakati kama njia ya kufanikisha maendeleo ya nchi na hadi kufikia 2025 Mkongo wa Taifa utakuwa umefikia Kilomita15,000 na kuunganisha mikoa na Wilaya zote.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL,) Mhandisi. Peter Ulanga amesema makubaliano hayo yataleta tija katika sekta mbalimbali pamoja na kukuza uhusiano wa kipiplomasia, uchumi na usalama.

Ameeleza kuwa, TTCL itatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa masharti ya mkataba huo ambao utachangia Maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Ulanga amesema, Uhusiano wa Tanzania na Burundi kupitia Burundi Backbone System ulianza mwaka 2019 kwa kuingia mkataba wa kwanza wa kuwapa huduma za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ambao
ulihusisha kuunganisha Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano na Mkongo wa
Burundi (BBS,) kupitia eneo la Kabanga mpakani mwa Tanzania na Burundi kupitia Wilaya za Ngara, Mkoa wa Kagera na Manyovu upande wa Kigoma.

“Matokeo mazuri ya huduma za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano yamepelekea Serikali ya Burundi, kupitia BBS, kukubali kuongeza huduma hizo. Mkataba mpya utaimarisha uhusiano wa kibiashara kati ya Tanzania na Burundi na utaboresha mawasiliano kati ya
nchi hizo mbili, Ukanda wa Afrika Mashariki na Nchi za Kusini mwa Afrika…..Tunaamini mkataba huu mpya utakuwa na manufaa makubwa kwa wananchi wa Tanzania na Burundi kwa kuimarisha uchumi, biashara, na ushirikiano wa kijamii….na tunawaalika pia kutumia fursa ya kutumia kituo cha kuhifadhi data cha Tanzania kwa kuhifadhi data zao.” Amesema

Pia, Mkurugenzi Mtendaji wa BSS Jeremie Diomede Hageringwe amesema mkataba huo utanufaisha Nchi zote mbili hususani katika upatikanaji wa huduma ya intaneti kwa urahisi.

“Upatikanaji wa huduma ya intaneti kwa urahisi, huduma bora na bei rahisi utachochea maendeleo ya biashara kwa wananchi kupitia mtandao na hii ni pamoja na utoaji huduma bora ambayo ni moja ya vipaumbele kwa Serikali ya Burundi.” Amesema.

Pia ameishukuru Serikali ya Tanzania kupitia Wizara husika na TTCL kwa kufanikisha mchakato huo kupitia majadiliano yenye tija kwa wananchi wa Tanzania na Burundi.
 Mkurugenzi Mkuu wa TTCL Mhandisi. Peter Ulanga (kushoto,) na Mtendaji Mkuu BBS (kulia,) wakisaini makubaliano hayo yanayoshuhudiwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania ( TCRA,) Dkt. Jabir Bakari na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TTCL Zuhura Muro.

Mtendaji Mkuu wa BBS Jeremie Diomede Hageringwe akizungumza wakati wa hafla hiyo na kuishukuru Serikali ya Tanzania kwa kufanikisha mchakato huo kupitia majadiliano yenye tija kwa wananchi wa Tanzania na Burundi. Leo jijini Dar es Salaam.


Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini mkataba wa kibiashara wa kuongeza huduma kwenye Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kati ya TTCL na BBS na kueleza kuwa Serikali imedhamiria kuboresha sekta ya mawasiliano ndani na nje ya mipaka ya Tanzania. Leo jijini Dar es Salaam.

Share To:

Post A Comment: