Mdau wa elimu na Mkurugenzi wa Msowoya Foundation, Dk Tumaini Msowoya amepata nafasi ya kuzungumza na wanafunzi wa kike wa Shule ya Sekondari Mbalamaziwa ambao wamempatia jina la Shangazi.

Katika mazungumzo hayo, Dkt Msowoya amewapa mbinu zitakazo wasaidia kuvuka vikwazo ili wafikie malengo yao kitaaluma na kutimiza ndoto zao kimaisha.

Amewataka wajifunze kusema ‘hapana’ na kutoa taarifa kwa walimu au walezi wanapokutana na watu wenye nia ovu ya kufukia ndoto zao ili kuepika mimba na ndoa za utotoni.

Dkt Msowoya amewataka kujiamini, kujilinda, kujipenda, kuwa na nidhamu, kusoma kwa bidii, kujituma kwenye kazi na kumcha Mungu kila mmoja kwa imani yake kama mbinu za kufikia ndoto zao kimaisha.

Aidha ameupongeza uongozi wa Shule kwa kuandaa mashindano ya usafi mabwenini unao wafanya wasichana hao kuwa na msingi imara utakao wasaidia hadi watakapo kuwa watu wazima.

“Nimeambiwa bweni safi na chumba kisafi huwa kinapewa zawadi ya mbuzi na nyingine. Huu ni ubunifu na kwa macho yangu nimeshuhudia usafi kwa kiwango cha juu mabwenini. Hongera mkuu na walimu kwa ubunifu,” amesema Dk Msowoya.

Awali, Mkuu wa Shule ya Sekondari Mbalamaziwa, Christom Lalika alisema lengo kubwa la shule hiyo ni kuongeza ufaulu kwa wanafunzi huku wakitilia mkazo suala la nidhamu.

Msowoya kupitia Msowoya Foundation ameanzisha kampeni inayoitwa Ng’ara kijana ikilenga kuwasaidia wanafunzi wa kike na kiume kufikia ndoto zao hasa kielimu.

Share To:

Post A Comment: