Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene amewataka watalaam wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kutatua changamoto wanazokutana nazo wananchi wanaotumia mifumo ya TEHAMA ili kurahisisha upatikanaji wa huduma.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa  kikao kazi cha nne cha Serikali Mtandao kinachofanyika kwa siku tatu mkoani humo kikiwa na kaulimbiu isemayo “Uzingatiaji wa Sera, Sheria, Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao kwa ubadilishanaji salama wa Taarifa”.

Sambamba na hilo pia  ameeleza kuwa  Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 na Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa miaka mitano kwa pamoja zinatambua nafasi ya TEHAMA katika kufikia malengo ya Taifa na zinasisitiza juu ya matumizi sahihi ya TEHAMA katika utekelezaji wa shughuli za serikali na utoaji wa huduma kwa wananchi.

“Rai yangu ni kwamba, ni lazima kuingia katika mifumo na kuihuisha kila siku kwa sababu katika kufanya hivyo, kunapunguza malalamiko ya wananchi. Ni vyema taasisi zote za umma tukawa mashabiki na kulazimishana kuingia kwenye matumizi ya mifumo kwa kuwa hatuwezi kwenda tofauti na teknolojia”, amesema Mhe. Simbachawene.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Selestine Kakele, amesema kuwa serikali yoyote ina wajibu wa kutunza ulinzi na usalama kwa watu wake na kutoa huduma kwa jamii, katika kutimiza wajibu wa utoaji huduma, Serikali inazingatia kutoa huduma kwa gharama nafuu, kwa uhakika na kuwafikia wengi hivyo, matumizi ya TEHAMA ni njia sahihi kwa serikali kuendelea kushusha huduma mbalimbali kwa wananchi.

“Tungekuwa vitani, ninyi Maafisa TEHAMA na wengine mnaotumia mifumo hiyo ndio jeshi letu, tungelitanguliza mbele kuhakikisha kwamba wajibu tuliopangiwa tunaweza kuufikia. Kwa niaba ya Wizara, tunaahidi kuendelea kushirikiana kujenga mifumo imara na endelevu ya TEHAMA ambayo itasaidia Serikali kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi”, amesema Kakele.

Share To:

Post A Comment: