Serikali ya awamu ya sita, katika kuhakikisha umeme unafika maeneo yote vijijini kwa lengo la kuchochea kasi ya maendeleo nchini na ukuaji wa wa uchumi, kupitia mradi wa umeme vijijini REA, imefanikiwa kusambaza umeme kwenye Kijiji cha Endagem kata ya Endabash, wilaya ya Karatu na hatimaye kufikisha kitongoji cha Maurus, eneo la machimbo ya Dhahabu Mgodi wa Endagem.

Wachimba hao wadogo wa madini ya dhahabu, katika mgodi huo, wameishukuru na kuipongeza serikali kwa kusikiliza na kutatua kero za wananchi, kwa kufikisha huduma hiyo kwenye mgodi huo, kero ambayo imedumu kwa miaka 12, kero ambayo waliiwasilisha kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe.John V.K Mongella Oktoba, 2023 na muda mfupi tayari umeme umefika eneo hilo.

Akizungumza kwa niaba ya wachimbaji hao, Mwenyekiti wa wachimbaji Madini ya dhahabu Mgodi wa Endagen, Abdul Amir Mwangu, amekiri uwepo wa rasilimali ya umeme eneo hilo, utaongeza kasi ya uchimbaji utakaokuza biashara na pato la mtu mmoja mmoja kwa wachimbaji hao, kwa kuwa sasa watachimba madini kwa kutumia mashine zenye teknolojia ya kisasa zinazotumia umeme, tofauti na hapo awali walichimba kwa mashine duni zilizotumia mafuta ya dizel ambazo zinatumia gharama kubwa za uendeshaji.

“Tunaishukuru Serikari ya Mama Samia, ametimiza haja na matamamio yetu ya miaka mingi, tulitoa kero yetu mwezi Oktoba, 2023 kwa mkuu wa Mkoa, muda mfupi tumepata umeme na transfoma mbili kubwa zimesimikwa eneo hili, tumeshuhudia Serikali ya awamu ya sita kuwa ni sikivu, tunaamini tunakwenda kuongeza kasi ya uzalishaji kwa kutumia mashine za kisasa, tumekuwa tukichimba kwa teknolojia dhaifu iliyozorotesha uzalishaji kwa sasa biashara zetu zinakwenda kukua”. Amesema Menyekiti Mwangu.

Hata hivyo wananchi hao, licha ya kuishukuru Serikali, wameiomba kujengewa shule ya msingi na zahanati kwa kuwa eneo hilo halina huduma hizo, jambo ambalo linawatesha wanawake wajawazito na watoto wadogo wasio na uwezo wa kutembea umbali mrefu kufuata shule kijiji cha Laja.

Mradi huo unaotekelezwa kwa shilingi milioni 545.3 na mkandarasi ETDCO kampuni tanzu ya TANESCO na umefikia asilimia 80.

Share To:

Post A Comment: