Na. John I. Bera – SAME


MKUU wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Nurdin Babu, ametoa rai kwa wataalamu wa misitu nchini kutoa elimu kwa wananchi juu ya fursa za misitu ikiwamo teknolojia ya hewa ukaa huku akimekemea tabia ya baadhi ya wafugaji kulisha mifugo yao miti inayopandwa na kusisitiza kutomvumilia kwa yeyote atakayekutwa akifanya hivyo.

Mhe. Babu ametoa rai hiyo leo Machi 19, 2024 Wilayani Same, Mkoa wa Kilimanjaro wakati akifungua warsha kuhusu masuala ya uhifadhi wa rasilimali za misitu ikiwa ni sehemu ya matukio kuelekea kwenye maadhimisho ya Siku ya Misitu Duniani na Siku ya Upandaji Miti Kitaifa inayofanyika Machi 21 wilayani Same, Kilimanjaro.

Amesema misitu imekuwa na manufaa mengi na kuwa fursa zake zimekuwa zikiongezeka ikiwamo teknolojia ya hewa ukaa na kuwa wananchi wakizitambua fursa hizo watahamasika katika utunzaji wa misitu kwa ajili ya fursa za kiuchumi.

“Misitu imekuwa na umuhimu mkubwa sana kwani inachangia asilimia 3 ya pato la taifa, vifaa vya ujenzi, upatikanaji wa mvua, kuzuia mmomoyoko wa udongo na makazi ya wanyama, na fursa zake pia zimekuwa zikiongezeka kila hadi siku, hivyo hatuna budi ya kuhakikisha misitu inahifadhiwa.”

“Elimu ikitolewe kwa wadau mara kwa mara na wananchi wakifahamu fursa zinazopatikana katika misitu watashiriki katika uhifadhi, hivyo wataalamu wa misitu hakikisheni mnaielimisha jamii katika hili.”

Babu amesema Wilaya ya Same ni miongoni mwa wilaya zilizoathirika na ukataji holela wa miti na kilimo kisichofuata taratibu ya mazingira hatua ambayo imechangia vifo vya watoto kutokana na maporomoko ya udongo.

“Same watu wanalima kandokando ya vyanzo vya maji na magema tumepoteza watoto wengi hasa kutokana na nyumba nyingi kujengwa china ya magema, barabara zinaharibika na wakulima wengine wanalima mahindi mpaka kwenye kingo na udongo unakuwa mwepesi na kuporomoka.”

Katika kuirejesha Wilaya ya Same na Mkoa wa Kilimanjaro kwa ujumla kuwa ya kijani, Mhe. Babu alimuagiza Katibu Tawala Mkoa huo kusimamia kwa ukaribu kampeni za upandaji miti ili ipandwe ya kutosha.

“Katibu Tawala wa Mkoa, lazima tukubaliane mtu anaruhusiwa kupanda miti lakini wanapotaka kukata lazima tujue mti uko wapi na unakatwa kwa shughuli gani.”

Babu amesema pia Serikali ya Mkoa wa Kilimajaro hautavumilia wafugaji wanaolisha mifugo yao miti ya serikali inayopandwa na kusisitiza atakayekamatwa akifanya hivyo basi mifugo hiyo itakuwa ni mali ya serikali.

Pia, amewataka maafisa ardhi kuhakikisha ya kutoa vibali vya ujenzi kwa mtu ambaye amepanda miti isiyopungua mitano na kumtaka Katibu Tawala wa Mkoa kulisimamia hilo.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Same, Mhe. Kasilda Mgeni alisema Wilaya ya Same imekuwa ikimuunga mkono Rais Mheshimiwa Rais Dkt. Samia kwa kuhakikisha wanahifadhi mazingira kwa kupanda miti ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Alisema katika kampeni ya kuifanya Same ya Kijani wamepanda miti kandokando ya barabara kuanzia mwanzo hadi mwisho wa wilaya na mpaka sasa zaidi ya miti laki tano imeshapandwa katika kampeni ya kuifanya Same kuwa ya kijani.

Aidha, mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii ambae pia ni Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Ufugaji Nyuki, Bw. Daniel Pancras amesema Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii inajukumu kubwa la kuhamasisha upandaji miti pamoja na kuelimisha juu ya upandaji miti ili watanzania wajue namna bora ya kupanda na kutunza miti


 

Share To:

ASHRACK

Post A Comment: