Na. Yussuf Abbas: Dodoma
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Raisi Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mh. Muhamed Mchengerwa (Mb) ametoa wito kwa halmashauri zote nchini kuiga mfano wa halmashauri ya Kwimba iliyoibuka kinara katika matumizi sahihi ya Mfumo wa kielektroniki wa Ununuzi wa Umma (NeST).
Mh. Mchengerwa ameyasema hayo leo jijini Dodoma akiwa Makao Makuu ya ofisi za TAMISEMI katika hafla ya utoaji tuzo hiyo iliyotolewa na Mamlakaa ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma PPRA kupitia Mkurugenzi wake Mkuu Bw. Eliakim Maswi.
Ameeleza kuwa hatua hii ni ishara ya weledi wa taasisi za umma katika kutii agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha Serikali inatekeleza majukumu yake kiutendaji kupitia mifumo ili kuleta ufanisi wa kazi sambamba na kupunguza gharama za matumizi na hatimae kuokoa fedha za Serikali.
“Nadhani tumeweza kumsikiliza Mkurugenzi hapa akieleza ni kwa namna gani Kupitia mfumo huu wameweza kupunguza gharama za matumizi, suala ambalo limeweza kuisaidia Serikali kuokoa fedha ambazo pengine zingetumika ndivyo sivyo” Amesema Mchengerwa
Mkurugenzi Mkuu wa PPRA Bw. Eliakim Maswi ameeleza kufurahishwa na Utendaji kazi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya hiyo ya Kwimba kwa na kusema kuwa watu wa aina hiyo ni watu wanaotenda majukumu yao kikamilifu na kuzingatia misingi na maadili ya kazi zao, hivyo wanapaswa kuzingatiwa kwa uchapakazi wao.
“Mh. Waziri unajua ilipo Halmashauri ya Kwimba ni pembeni, Lakini pamoja na kuwa pembeni alichokifanya Mkurugenzi wa Kwimba sisi kama Mamlaka tumefurahishwa sana na utendaji wake tukaona tuje kumsema mbele yako kuwa huyu Mkurugenzi anatufanyia kazi nzuri bila kulalamika kuwa mfumo unamsumbua” Alieleza Maswi.
Nae Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kwembe Bi. Happiness Joachim Msanga ameeleza kuwa siri ya mafanikio hayo waliyoyapata kwa kipindi hiki kifupi tangu kuanzishwa kwa mfumo wa NeST ni pamoja na kujizatiti katika ufanya kazi kwa kutoa elimu ya kutosha kwa watumishi wote walio kwenye mipaka ya halmashauri kuhusu matumizi ya Mfumo wa Ununuzi, Elimu hiyo ilijumuisha uwezeshaji wa Mkuu wa wilya, wajumbe wa kamati ya usalama, katibu wa chama sambamba na watumishi wa makundi wakiwemo Walimu Wakuu wa Shule za Msingi na Sekondari, Wakuu wa Vituo vya Afya na zahanati pamoja na watendaji wa kata na vijiji.
Bi. Happiness ametaja njia nyingine ni pamoja na kutoa msada kwa wa kufanya maombi ya tenda kwa wazabuni wasiokuwa na uelewa wa kutosha kuhusu matumizi ya mfumo wa NeST kwa kuwapa msaada kupitia watu wa Ununuzi sambamba na wataalamu wa TEHAMA.
Aidha ameongezea kuwa kupitia Mfumo wa NeST umewasaidia sana kwenye mambo mengi ya Ununuzi ikiwa ni pamoja na kushuka kwa gharama za bidhaa na kupunguza migogoro na lawama za upatikanaji wa tenda.
“ Sasahivi kupitia Mfumo hakuna mtumishi anaekuja kulalamika kuwa mtu wake hajapata tenda wala Mfanya biashara kutokana uwepo wa uwazi kwenye mfumo, maana kupitia mfumo sasa hata mzabuni mzabuni ambaye hajashinda ataona sababu ya kwanini hakushinda na aliyeshinda ataona sababu iliyompelekea kushinda” Alimalizia
Halmashauri ya Kwimba imejinyakulia tuzo hiyo ya kiasi cha Shilingi Milioni 10 kwa kuwa Taasisi ya umma kinara katika matumizi ya mfumo wa NeST katika kufanya Ununuzi kufuatia kutangaza zabuni nyingi zaidi kuliko taasisi nunuzi yoyote serikalini. Jumla ya zabuni ilizotangaza mpaka leo asubuhi ni 472 ikifuatiwa na Halmashauri na Ngara iliyotangaza jumla ya zabuni 150 sambamba na Halmashauri ya Mbarali ambayo imetangaza zabuni 141.
Waziri wa TAMISEMI Mh. Mohamed Mchengerwa akikabidhi zawadi ya kiasi cha Sh. Milioni 10 kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kwembe Bi. Happiness  Msanga Walioibuka kinara kuwa Taasisi iliyofanya vizuri kitaifa katika matumizi ya Mfumo wa NeST.
Waziri wa TAMISEMI Mh. Mohamed Mchengerwa akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa PPRA Eliakimu Maswi wakati wa Waziri huyo akikabidhi zawadi ya kiasi cha Sh. Milioni 10 kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kwembe Bi. Happiness  Msanga Walioibuka kinara kuwa Taasisi iliyofanya vizuri kitaifa katika matumizi ya Mfumo wa NeST.
Share To:

Post A Comment: