Hamasa ya wananchi wanaojiandikisha kuhama kwa hiyari kutoka eneo la hifadhi ya Ngorongoro imeongezeka ambapo jumla ya kaya 82 zenye wananchi 541 na mifugo 3,379 zimehama kutoka Ngorongoro kweda Kijiji cha Msomera Handeni Tanga.

Akizungumza wakati wa kuaga kundi hilo Kamishna wa Uhifadhi wa NCAA Richard Kiiza amesema kuwa baada ya kuhama kwa kundi hilo leo inafanya idadi ya wananchi waliokwishahama ndani ya hifadhi tangu zoezi lilipoanza hadi leo kufikia kaya 1,032 zenye watu 6,395 na mifugo 28,982.

Kamishna Kiiza amebainisha kuwa kadri siku zinavyoenda wananchi wengi wanahamasika na kujiandikisha kuhama kwa hiari yao wenyewe hasa baada ya ushuhuda wa maisha mazuri kwa wananchi wenzao waliokwishatangulia ambao Maisha yao yamebadilika kwa kiasi kikubwa.

“Wananchi waliotangulia mwaka jana wengi wao wamejenga nyumba za kisasa, wamelima mazao ya kutosha kwa ajili ya chakula na biashara, wanamiliki vyombo vya usafiri, wanapata huduma bora za maji, umeme, shule, mawasiliano, huduma za afya, posta, malisho na majosho, hali hii imefanya wao kuwa mabalozi kwa wenzao waliobaki Ngorongoro” ameongeza Kiiza.

Kiiza ameongeza kuwa wananchi ambao walikuwa hawajajiandikisha wamegundua walikuwa wanapotoshwa na baadhi ya watu ambao hawaishi ndani ya hifadhi, bila kujua changamoto wanazokutana nazo wananchi za kushambuliwa na Wanyama wakali na kushindwa kufanya baadhi ya shughuli za kiuchumi kutokana na sheria za hifadhi.

Kwa upande wake mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro Kanali Wilson Sakulo akiwaaga wananchi hao ameeeleza kuwa wananchi wote wanaohama haki zao za msingi zimezingatiwa kwa mujibu wa sheria, na kila kaya inayoondoka inaingiziwa fedha kiasi cha shilingi milioni 10 na fedha zingine za fidia ya maendelezo waliyoyafanya wakiwa Ngorongoro.

Share To:

Post A Comment: