Mkuu wa mkoa wa Manyara, Queen Cuthbert Sendiga amesema huduma za afya zimeboreshwa hivi sasa eneo hilo ndiyo sababu wagonjwa na majeruhi wa maafa yaliyotokea Hanang' walitibiwa Manyara.


Maporomoko ya tope kutoka mlima Hanang' yalitokea Desemba 3 mwaka 2023 na kusababisha vifo vya watu 89, wengine kujeruhiwa na wengine kukosa makazi.

Maafa hayo yalitokea jumapili alfajiri na kuathiri miundombinu ya mji mdogo wa Katesh na maeneo ya karibu ya Gendabi, Jorodom, Ganana, Sarijandu na Dumbeta.

Sendiga akizungumza mjini Babati kwenye kikao cha ushauri cha mkoa huo (RCC) amesema wagonjwa na majeruhi, walitibiwa Manyara kwani hawakusafirishwa ila madaktari bingwa ndiyo walikuja Manyara.

Amesema wagonjwa na majeruhi wa maafa ya Hanang' walitibiwa Manyara, kutokana na huduma bora za afya kuboreshwa ikiwemo kuwepo kwa vifaa tiba na dawa.

"Tukiwa tunaadhimisha miaka mitatu ya uongozi wa serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, kwa upande wetu mkoa wa Manyara, tumepiga hatua kubwa atika sekta ya afya," amesema Sendiga.

Amesema mara baada ya tukio hilo wagonjwa na majeruhi wa maafa hayo walipatiwa matibabu kwenye hospitali ya wilaya ya Hanang' (Tumaini).

Amesema wagonjwa na majeruhi wengine walipatiwa rufaa kwenye hospitali ya mkoa wa Manyara iliyopo mjini Babati hivyo hawakutoka nje ya Manyara.

"Wataalamu wa tiba tuu wakiwemo madaktari bingwa ndiyo walitoka nje ya Manyara, ila kwa upande wa dawa na vifaa tiba tupo vizuri, ndiyo sababu wagonjwa na majeruhi wote walitibiwa hapa kwetu," amesema Sendiga.

Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Hanang' Rose Kamili amemshukuru mkuu huyo wa mkoa kwa namna alivyoshiriki ipasavyo katika maafa hayo.

"Tunakushukuru wewe na viongozi wengine wa mkoa huu na wilaya nyingine kwa namna mlivyotukumbatia mara baada ya sisi kupatwa na maafa hayo yaliyoondoka na wapendwa wetu," amesema Kamili.
Share To:

Post A Comment: