Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea kuboresha sekta ya afya kwa kutoa magari mawili ya kubebea wagonjwa kwa Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) ya jijini Dodoma ili kusaidia wagonjwa wa kanda ya kati kufika kwa wakati Hospitalini.

Akizungumza baada ya hafla ya kupokea magari hayo, Mbunge wa Dodoma mjini, Mhe. Anthony Mavunde, amesema magari hayo yataondoa changamoto ya wagonjwa wanapopata rufaa.

“Naishukuru Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kuboresha sekta ya afya na kuweka mazingira rafiki kwa wananchi kupata Huduma bora za afya”,amemshukuru Mhe. Mavunde.

Ameongeza kuwa magari ya kubebea wagonjwa ni muhimu sana kwa BMH kwani Hospitali hii imekuwa kimbilio sio tu kwa wakazi wa Dodoma na kanda ya kati bali kwa watanzania kwa ujumla.

“Tutasimamia magari haya yatumike kwa malengo yaliyokusudiwa ambayo ni kubeba wagonjwa ,” amesisitiza Mhe. Senyamule

Nitajitahidi kwa nafasi yangu kuhakikisha tunaongeza gari lingine la wagonjwa kwa kuwa hospital hii inahudumia watu wengi zaidi ya hospital nyingi za hapa Dodoma hivyo ni muhimu kuboresha eneo hili”Alisema Mavunde

Akitoa maelezo ya awali Mkurugenzi Mtendaji wa Hospital ya Benjamin Mkapa Dkt. Alphonce Chandika amesema magari hayo yatasaidia sana katika kusafirisha wagonjwa wa rufaa kutoka Hospitalini hapo na hivyo kutumia fursa hiyo kuishukuru sana serikali kwa magari hayo ya kisasa na yenye vifaa muhimu vya matibabu ambayo yatarahisisha utoaji huduma kwa wagonjwa.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mh. Rosemary Senyamule amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maboresho makubwa ya sekta ya Afya mkoani Dodoma na kuutaka uongozi wa Hospitali ya Benjamin Mkapa kuyatunza magari hayo na kuhakikisha yanafanya kazi iliyokusudiwa.





Share To:

Post A Comment: