Na.Samwel Mtuwa - Tanga
Naibu Waziri wa Madini Dkt.Steven Kiruswa leo Januari 16, 2023 ametembelea kiwanda cha kuchakata na kuzalisha madini ya kinywe kilichopo wilaya ya Handeni mkoani Tanga ambapo ameshuhudia shughuli mbalimbali za uzalishaji zikiendelea.
Akizungumza katika mkutano na wafanyakazi wa kiwanda pamoja na Uongozi , Dkt.Kiruswa amefafanua kuwa serikali inaandaa mpango mkakati utakaoelekeza katika mnyororo mzima wa shughuli za uchimbaji na uchakataji wa madini mkakati wenye lengo la kuhakikisha shughuli zote za uchakataji zinafanyikia hapa nchini.
Naye , Mkurugenzi wa kiwanda hicho Godlisten Mwanga ambaye ni Mtanzania amesema kuwa uzalishaji rasmi wa madini ya kinywe ulianza mwaka 2021 ambapo kufikia mwaka 2023 kiwanda kimefanikiwa kuzalisha jumla ya tani 22,357.
Mwanga ameongeza kuwa mpango wa awali ulikuwa kuzalisha tani 78,000 lakini kutokana na changamoto za nishati ya umeme na miundombinu ya barabara imeshindikana kufikia wastani huo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Handeni Wakili Albert Msando amesema kuwa kiasi cha bilioni 50 tayari kimetengwa kwa ajili ya kusimika mitambo ya uzalishaji wa nishati ya umeme itakayo elekezwa katika sehemu za migodi ya uzalishaji madini.
Post A Comment: