Na Happiness Shayo - Kilimanjaro 


Waziri wa Maliasili na Utalii,  Mhe. Angellah Kairuki (Mb) amewatunuku vyeti  wapanda mlima Kilimanjaro 228  walioshiriki  kampeni ya " Twenzetu Kileleni 2023" kwa ajili ya kuadhimisha miaka 62 ya Uhuru wa Tanganyika Desemba 9,2023.

Hafla ya mapokezi ya wapanda mlima,waliopanda kuadhimisha miaka 62 ya Uhuru wa Tanganyika  na kushuka tarehe 10 Desemba 2023 imefanyika  katika lango la Marangu, Mkoani Kilimanjaro.

"Niendelee kuwapongeza wapandaji wote kufanikisha zoezi la "Twenzetu Kileleni 2023" na kusimika Bendera ya Taifa katika Kilele cha Mlima Kilimanjaro ili kusherehekea miaka 62 ya uhuru wa Tanganyika" Mhe. Kairuki alisisitiza. 

Amefafanua kuwa zoezi la kupanda mlima ili kuadhimisha uhuru wa Tanganyika limeendelea kuvuta hisia za watu wengi ikiwemo Waheshimiwa Mabalozi wa Tanzania kutaka kushiriki kupanda mlima huo.

Amesema lengo ni kujua vivutio vilivyomo na kwenda kuvinadi katika nchi wanazoiwakilisha Tanzania hivyo ujio wao una manufaa makubwa kwa Taifa la Tanzania. 

Amewataka Mabalozi hao kuendelea kuvinadi vivutio vya utalii vilivyoko nchini ili dhamira ya Serikali ya kuwa na idadi ya watalii milioni 5 ifikapo 2025 iweze kutimia.

Aidha, ametoa rai kwa Watanzania na wananchi wote kufuata sheria na kutovamia maeneo yaliyohifadhiwa kwani, kwa kufanya hivyo ni kuhujumu rasilimali za nchi.

Hafla hiyo iliyokuwa na kaulimbiu ya " Tunza mazingira ya ukanda wa Pwani okoa barafu ya Mlima Kilimanjaro"  imetilia msisitizo Watanzania na dunia kwa ujumla kulinda mazingira ili kuepukana na vitendo vya ukataji miti holela ili kusaidia kurudisha uoto wa asili na hali nzuri ya hewa ambayo ni tunu katika kuendeleza uwepo wa Barafu ya Mlima Kilimanjaro.

Zoezi la kupanda kupanda mlima lilihusisha wawakilishi kutoka Taasisi za Serikali, Taasisi Binafsi, Watu Binafsi pamoja na Wanahabari.

Share To:

Post A Comment: