Na Munir Shemweta, WANMM HANANG

 

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Mizengo Pinda ametembelea maeneo yaliyoathirika Mafuriko yaliyotokana na maporomoko ya mawe na tope kutoka mlima Hanang.

 

Mhe. Pinda ametembelea maeneo hayo tarehe 20 Desemba 2023 kabla ya kuhudhuria kikao cha Utekelezaji Maagizo kuhusu Mafuriko yaliyotokana na maporomoko ya mawe na tope kutoka mlima Hanang.

 

Naibu Waziri Pinda alitembelea maeneo yaliyoathirika kwenye mji wa Katesh pamoja na kijiji cha Gendabi mkoani Manyara.

 

Akiwa katika maeneo hayo Mhe Pinda alikutana na Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge, Sera na Uratibu) Jenister Mhagama aliyekwenda kutembelea maeneo mbalimbali katika halmashauri ya Hanang kujionea urejeshaji wa hali katika maeneo yaliyoathiriwa na maafa ya maporomoko na tope na mawe mlima Hanang.

 

Wakiwa katika maeneo ya waathirika, Mawaziri walijionea hali halisi ya urejeshaji hali katika maeneo yaliyoathirika na maafa pamoja na kukagua ugawaji misaada kwa wananchi walioathirika na maafa.

 

Baadhi ya Wananchi waliozungumza na Mawaziri hao wameeleza kuridhishwa kwao na juhudi za serikali hasa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan katika kuwasaidia wale waliokumbwa na athari ya mafuriko katika eneo hilo.

 

‘’Tunaomba mtupelekee salamu na shukran zetu kwa Rais Samia kutokana na juhudi zake na jinsi alivyolipa uzito suala hili la waathirika wa mafuriko, tumhakikishie tuko pamoja naye’’ walisema.

 

Mafuriko yaliyotokana na maporomoko ya mawe na tope kutoka mlima Hanang yamesababisha jumla ya wananchi 87 miili yao kupatikana baada ya kupoteza maisha na majeruhi kuendelea kupata matibabu katika hospitali ya Hydom, wilaya na mkoa. Sambamba na hilo baadhi ya wananchi wanaendelea kupata hifadhi katika maeneo ya taasisisi za elimu zilizopo Katesh baada ya makazi yao kuharibiwa.

Share To:

TANGA RAHA BLOG

Post A Comment: