Na Zuena Msuya na Issa Sabuni, Dar es Salaam
Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga kwa niaba ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amepokea Magari 21 yenye thamani ya shilingili Bilioni 1.9 kutoka Umoja wa Ulaya (EU) kwa ajili ya kuimarisha usimamizi wa Miradi ya Nishati Vijijini.
Mhe. Kapinga amepokea magari hayo katika Ofisi ndogo ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) jijini Dar es salaam ambapo pamoja na mambo mengine amewasihi REA kuyatunza magari hayo na kuyatumia kwa kazi iliyokusudiwa.
Amesema magari hayo yatumike kusaidia kusambaza umeme kwa Watanzania na watambue kuwa Wadau wanapounga mkono jitihada za Serikali ni wajibu kuhakikisha kuwa rasilimali hizo zinatumika kwa uaminifu na weledi mkubwa ili kuwaletea Watanzania maendeleo.
Amesema Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko, amekuwa akitoa miongozo kila wakati kusimamia miradi hiyo kwa weledi mkubwa ili kuleta ufanisi na fedha inayowekwa kwenye miradi hiyo iwanufaishe watanzania na wapate umeme wa uhakika ambao unaboresha Maisha yao ya kiuchumi.
“EU wamekuwa Wadau wetu wa muda mrefu na wamekuwa wakiunga mikono miradi mbalimbali nchini ikiwemo hii ya nishati kwa ajili ya kuboresha maisha ya Watanzania, tunaamini mashirikiano haya yataendelea baina yetu sisi na kujenga umoja kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya katika kuendelea na kuwaletea Watanzania maendeleo”, alisema Mhe. Kapinga.
Amesema EU wamekuwa wakikunga mkono miradi mbalimbali ambayo inatekelezwa kupitia Wizara na Taasisi zake ikiwemo za REA wa Usambazaji wa Umeme Vijijini na Shirika la Umeme nchini Tanzania (TANESCO) kupitia mradi wa Tanzania na Zambia (TAZA).
Tunaendelea kumshukuru Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa anaoufanya katika Sekta ya Nishati kwa kutoa fedha ambazo zinatumika kwenye miradi inayochini ya Wizara na Taasisi zake, ambapo mpaka sasa takribani Vijiji Elfu 11 viunganishwa na umeme na vichache vililivyosalia vinatarajia kumalizika mwezi Juni 2024.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Balozi wa EU nchini Tanzania, Cedric Merej amesema EU imetoa magari hayo kwa kutambua usimamizi mzuri wa fedha na misaada mbalimbali inayotolewa na umoja huo kwa ajili wa kutekeleza miradi ya Nishati kwa watanzania ambayo imekuwa ikiwafikia walengwa kama ilivyokusudiwa.
Ameipongeza Wizara ya Nishati kupitia REA kuendelea kutekeleza Miradi ya Nishati Vijijini na ameahidi kuendelea kuunga mkono jitihada za Serikali katika azma yake ya kusambaza umeme katika kila kijiiji na Kitongoji.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy ameahidi kuwa magari hayo yatatatumika kama ilivyokusudiwa na kwamba yataongeza kasi na kurahisisha kazi ya kusambaza umeme vijijini.
‘’EU wamekuwa wakiunga mkono miradi mbalimbali ikiwemo mradi wa REA III (Mzunguko wa Kwanza, Ujazilizi, Kituo cha kupoza umeme cha Ifakara ambacho kimekamilika hivi karibuni na kuanza kufanya kazi, ujenzi wa miundombinu katika wilaya za Kilombero na Ulanga na Mradi maalum wa kupeleka umeme kwenye vituo vya afya na pampu za maji"
“Tunampongeza, Rais Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kujenga imani kwa Wabia wa Maendeleo na kuweza kutoa fedha na kuunga mkono miradi ya ndani, fedha za wenzetu hazitoki hivihivi wanazitoa sehemu ambao wanaona zinaenda kufanya kazi iliyokusudiwa na usimamizi wake uko makini” alisema, Mhandisi Saidy.
Ameahidi kuwa magari hayo yatatunzwa na yatatumika kwa uangalifu kuhakikisha yanasaidia katika kuongeza usimamizi ili kuharakisha utekelezaji wa Miradi ya Nishati Vijijini na Mradi wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia.
Post A Comment: