Serikali kupitia chuo Kikuu cha Dodoma inatarajia kuanza ujenzi wa kampasi ya chuo hicho mkoani Njombe ambapo tayari kiasi cha Dola Milioni nane zinazokaribia Bilioni 18 kwa fedha ya Tanzania tayari imetengwa ili kufanikisha mradi huo katika mkoa wa Njombe ikiwa ni kilio na maombi ya muda mrefu ya wananchi wa mkoa huo.


Makamu mkuu wa Chuo kikuu cha Dodoma Prof.Lughamo Kusiluka amebainisha hayo kwenye kikao cha ushauri cha mkoa wa Njombe (RCC) ambapo amesema kutokana na vigezo vya mradi,uongozi wa chuo hicho umependekeza makao makuu ya kampasi ya Chuo kikuu cha Dodoma mkoa wa Njombe yajengwe katika eneo lililotengwa Njombe mjini lililopo karibu na shule ya sekondari Njombe (NJOSS) lenye ukubwa wa ekari 110 huku pia wakipendekeza eneo la Ihalula lenye ukubwa wa ekari 320 liweze pia kutumiwa na chuo kwa ajili ya mafunzo.

"Sisi tunapendekeza kwa mamlaka na uongozi wa mkoa wa Njombe kwamba makao makuu ya kampasi ya chuo kikuu cha Dodoma mkoa wa Njombe iwe katika eneo hili lililopo mjini lakini lile eneo lililopo katika kijiji cha Ihalula lenye ekari 320 pia itolewe kwa ajili ya ujenzi wa kampasi kwasababu program ambazo tunategemea kuzianza ni zile ambazo zinaakisi shughuli za kiuchumi na kijamii za mkoa huu ni mikoa jirani"amesema Kusiluka

Dkt.Evaristo Mtitu ni mratibu msaidizi wa mradi wa elimu ya juu kwa mageuzi ya uchumi,amesema mradi huo ni wa miaka sita ambapo matarajio ni kuwa mwaka 2026 chuo hicho kiweze kuanza kufanya kazi "Tunaomba ushirikiano wa wananchi ili UDOM wasikwame kwa kuwa mradi huu ni wa miaka sita 2021 - 2026 chuo kinatakiwa kiwe kimesimama na kinafanya kazi"amesema Mtitu

Mkuu wa mkoa wa Njombe Anthony Mtaka kwa niaba ya serikali ya mkoa huo amehakikisha ushirikiano wa kutosha kwa kuwa wananchi wa mkoa wa Njombe wamekuwa na shauku ya muda mrefu kuona mkoa huo unakuwa na Chuo kikuu huku akimshukuru Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kusikikiza na kujali maombi ya wananchi wa Njombe.




 
Share To:

Post A Comment: