Kampuni ya ALAF Limited inayjihusisha na utengenezaji wa mabati ya aina mbalimbali imetoa msaada ya mabati 2000 yenye thamani ya Tsh milioni 50 kusaidia familia zilizoathirika na maporomoko ya tope kutoka Mlima Hanag katika wilaya ya Hanag Mkoa wa Manyara hivi karibuni.

Akipokea msaada huo, Mkuu wa Wilaya ya Hanang, Mh. Janet Mahanja aliishukuru ALAF Limited na kusema kuwa massada huo umekuja wakati mwafaka wakiwa wanajiandaa kuanza shughuli ya ujenzi wa makazi mbadala kwa walioathirika na janga hilo.

“Kuna waliopoteza makazi kabisa kwa hivyo mabati haya yatasaidia kuwajengea makazi mapya, alisema Mh. Mahanja na kusema ALAF imeitikia mwito wa Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa vitendo.

Alitoa wito kwa makampuni na mashirika mengine yaige mfano huu wa ALAF na wengine ambao tayari wameshatoa misaada mbalimbali kwa waathirika wa janga hilo.

Naye Meneja Mawasiliano wa ALAF, Theresia Mmasy alisema wao kama sehemu ya jamii, wametoa mabati hayo ili kusaidia wananchi wa Hanag kurejea katika hali yao ya kawaida baada ya janga hilo la maporomoko ya tope kutoka Mlima Hanag.

“Leo tumetoa mabati  2000 yenye thamani ya Tsh milioni 50 lakini tutaendelea kutoa ushirikiano pale ambapo tutahitajika kufanya hivyo,” alisema.

Kwa niaba ya kampuni ya ALAF alitoa pole kwa wote waliopoteza wapendwa wao na wengine kujeruhiwa katika janga hilo huku wengine wakipoteza makazi yao kabisa.
Share To:

Post A Comment: