Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amaeiagiza Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) kushirikiana na Taasisi Ya Wahandisi Tanzania (IET) Kuweka utaratibu endelevu wa kuwajengea uwezo Wahandisi ili waweze kuendana na mabadiliko ya teknolojia.

Bashungwa ameagiza hayo leo tarehe 30 Novemba wakati akifungua Kongamano la Kitaifa la 32 la Taasisi ya Wahandisi Tanzania lililofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere Arusha (AICC).

“Kutokana na asili ya tasnia ya uhandisi, Mhandisi ni mwanafunzi maisha yake yote,ninawaagiza ERB wakiungwa mkono na IET kuweka mpango maalumu wa kuwapatia ujuzi Wahandisi wetu walioko kazini kwa kutumia miradi iliyopo” amesema Bashungwa 

Bashungwa ameitaka Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) kupitia upya vigezo vya usajili wa Wahandisi kwa kufungua milango na kuondoa vikwazo visivyo vya lazima katika usajili.

“Idadi ya Wahandisi mahiri inatakiwa kuwa muhandisi mmoja kati ya wananchi 5,000, kwa hesabu za haraka, tunatakiwa kuwa na wahandisi mahiri zaidi ya 12,000 lakini nimeambiwa wahandisi washauri waelekezi ni chini ya 500”

Aidha, Bashungwa amesema azma ya Serikali chini ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kujenga uchumi ulio imara, imejiegemeza kwa kiwango kikubwa kwenye uwezo, juhudi, maarifa, weledi, nidhamu, umakini na ufanisi wa wataalam katika suala zima la utendaji kazi. 

Bashungwa ameeleza kuwa Wahandisi wabobezi wana deni la kuwalea na kuwaongoza wahandisi wachanga  ili waweze kuishi ndoto zao. 

Kadhalika, Bashungwa amewataka Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) pamoja na Taasisi Ya Wahandisi Tanzania (IET) kushirikiana kwa pamoja kutatua changamoto zinazoikabili tasnia ya uhandisi.

Bashungwa amewaagiza Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC), Bodi ya Makandarasi (CRB), Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) pamoja na Bodi ya Wakadiriaji Majengo (AQRB) kukamilisha mpango wa kushirikisha wataalamu wa ndani kuuwasilisha wizarani mpango kazi wa utekelezaji wa maagizo yote yaliyotolewa katika kikao tulichokaa na masuala ya ujenzi. 

Waziri Bashungwa amemwakilisha Waziri Mkuu, Mhe. Kasim Majaliwa Majaliwa (Mb.) ambaye alitarajiwa kuwa Mgeni rasmi katika ufunguzi wa Kongamano la Kitaifa la 32 la Taasisi ya Wahandisi Tanzania lililokuwa na Maudhui “Ubunifu unaotoa Suluhisho katika Uhandisi kwa Maendeleo Endelevu”.

Imetolewa na Kitengo cha Habari na Mawasiliano Serikalini Wizara ya Ujenzi.qq¹

Share To:

Post A Comment: