Na Happiness Shayo -Dodoma


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameruhusu kuanzishwa kwa mchakato wa kurejesha  kumbukumbu na vifaa vya jadi na utamaduni vinavyohusiana na historia ya Tanzania akiwemo mjusi mkubwa aina ya  Dinosaur aliyeko nchini Ujerumani ambaye ni kivutio kikubwa cha utalii nchini humo.

Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) alipokuwa akitoa taarifa kuhusu hoja ya Mhe. Riziki Lulida aliyetaka kujua  lini Serikali ya Tanzania itanufaika na mapato yatokanayo na mjusi aina ya Dinosaur ambapo Ujerumani inapokea mapato ya takriban dola bilioni 3.8 kama faida inayotokana na maonyesho ya mjusi huyo aliyeko katika Makumbusho ya Ujerumani.

“Nikuhakikishie tayari kama Serikali kupitia mazungumzo ya Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyoyafanya na Rais wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeir tunayo kamati ya kiserikali yenye taasisi zaidi ya nane ambayo itasimamia suala hili na baadae tutaendelea na majadiliano ambayo mheshimiwa Rais ametoa baraka zake” Mhe. Kairuki amesisitiza.

Hatua hiyo ya  mazungumzo baina ya nchi hizo mbili   inakuja ikiwa takribani wiki mbili sasa tangu Rais wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeir alipofanya ziara ya kikazi nchini Tanzania.

Amefafanua kuwa Serikali iko katika taratibu za kidiplomasia kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ili mazungumzo rasmi yaanze kuhusiana na 'artifacts' zote na vifaa vingine ambavyo ni kwa ajili ya kumbukumbu ya Tanzania ikiwemo mjusi pamoja na mengineyo.

Kwa upande wake Mhe. Lulida alifafanua kuwa kutokana mapato inayopata Ujerumani kwa kumuonyesha mjusi huyo, Serikali ya Tanzania inaweza kupata gawio ili iweze kuliendeleza  eneo la Tendaguru Mkoani Lindi ambako mjusi huyo alikochukuliwa.

Share To:

Post A Comment: