NAIBU Waziri anayeshughulikia Afya Ofisi ya Rais-TAMISEMI , Mhe Dkt. Festo Dugange amesema Serikali katika mwaka wa fedha wa 2023/24  imetenga kiasi cha Sh Milioni 900 kwa ajili ya ukarabati wa Hospitali Kongwe ya Mbozi.

Mhe. Dkt Dugange ameyasema hayo leo bungeni jijini Dodoma wakati akijibu maswali ya wabunge katika kikao cha saba mkutano wa 13 wa Bunge unaoendelea.

Amesema moja ya kipaumbele cha Serikali katika sekta ya afya ni kupunguza vifo vya wajawazito, watoto chini ya miaka mitano na watoto wachanga kwenye vituo vya kutolea huduma ya afya ya msingi.

" Katika mwaka wa fedha wa 2023/24 Serikali imetenga kiasi cha Sh Milioni 900 kwa ajili ya ukarabati wa Hospitali kongwe ya Mbozi. Pamoja na ukarabati na ujenzi wa miundombinu utakaofanyika katika hospitali ya Halmashauri ya Mbozi kipaumbele kimewekwa kwenye jengo la huduma za mama na mtoto ikiwemo huduma ya watoto njiti," Amesema Dkt Dugange.

Sanjari na hilo, Mhe Naibu Waziri Dkt Dugange amesema Kituo cha Afya cha Kinyangiri na Mkalama vilivyopo Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama ni miongoni mwa vituo 199 chakavu ambavyo Ofisi ya Rais-TAMISEMI imevianisha kwa ajili ya kuvitafutia fedha na kuvifanyia ukarabati na upanuzi.

" Serikali itaendelea kutenga bajeti kwa ajili ya ukarabati na kuongeza majengo kwenye vituo vya afya chakavu kote nchini na vituo hivi vya Kinyangiri na Mkalama vitapewa kipaumbele kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya upasuaji na wodi mara fedha zitakapopatikana," Amesema Mhe Dkt Dugange.

Share To:

Post A Comment: