Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Serikali ya Marekani, kupitia Shirika la Mandeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID) na Mpango wa Rais wa Marekani wa Kupambana na Malaria (PMI), imekabidhi Hadubini 133 na vitendanishi vingine vya maabara vyenye thamani ya zaidi ya Shilingi za kitanzania Bilioni 1.2 kwa ajili ya kutumika kufundishia katika vyuo vya Wizara ya Afya vinavyo toa kozi za maabara katika Mikoa sita ambayo ni Mbeya, Morogoro, Dar es Salaam, Tanga, Mara, na Singida.


Hafla ya makabidhiano ya vifaa hivyo iliyofanyika Novemba 13, 2023 katika chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUCOHAS) Jijini Dar es Salaam na kushuhudiwa na Mkuu wa Program kutoka Wizara ya Afya Dkt. Catherine Joachim akimuwakilisha Mganga Mkuu wa Serikali.

Dkt. Catherine amesema Hadubini hizo zitasaidia kukuza uwezo wa wataalamu wa maabara kwa kuweza kutambua kwa usahihi vimelea vya malaria kwa kuthibitisha uwepo wa vimelea hivyo ili kuwezesha wataalam wa afya kuanza matibabu sahihi na kwa haraka

"Hadubini hizi na vitendanishi vingine vya maabara vilivyotolewa leo vitawezesha Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Malaria kuimarisha uwezo wa kimaabara katika chunguzi na kusaidia utoaji matibabu ipasavyo, itakayopelekea kuokoa maisha ya watu na kuzuia madhara ya malaria". Amesema Dkt Catherine

Aidha Dkt. Catherine Amesema hadubini hizo zitatumika pia kufanya tafiti za kupima ufanisi wa dawa zinazotumika kutibu Malaria na ugunduzi wa mapema wa usugu wa dawa ili kuweza kubadili mikakati ya matibabu kwa wakati na kuzuia usugu usienee ili kuhakikisha kuwa dawa za malaria zinazotibu zinaendelea kupatikana kwa watu wote.

Nae Meneja Mpango wa wa Taifa wa Kudhibiti Malaria Dkt. Samwel Lazaro ameishukuru Serikali ya marekani kwa kupata hadubini kwenda kwenye vyuo vya afya kwani ndio asilimia kubwa wana ajiriwa kwenye vituo vya kutolea huduma za Afya

"Vifaa hivi vitasaidia sana katika kupata mafunzo na kuhakikisha wanafunzi wanapokuwa wanamaliza na kupata ajira kwenye vituo vya kutolea huduma za afya tutakuwa na uhakika na weledi wao na kuwezesha vipimo vya Malaria kufanyika kwa usahihi na kwa uhakika katika vituo hivyo". Amesema

Kwa upande wake Mkurugenzi wa ofisi ya Afya kutoka USAID Tanzania Bi.Anne Murphy ameipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Wizara ya Afya kwa juhudi zake zilizopelekea kupungua kwa kasi kiwango cha malaria nchini Tanzania kutoka zaidi ya asilimia 14 ya watu mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 8 tu mwaka 2022. 






Share To:

Post A Comment: