Wachimbaji wadogo wa Madini ya Dhahabu katika Mgodi wa Endagen ulioko kitongoji cha Murus kata Endabash wilaya ya Karatu mkoani Arusha wamewasilisha kero zao tano na kuiomba Serikali kuzitatua ili waweze kufanyakazi kazi kwa uhuru na kujipatia kipato. 

Wachimbaji hao wamewasilisha kero hizo kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. John V.K.Mongella alipofika kwenye mgodi huo kwa lengo la kukagua maendeleo ya mradi wa umeme katika eneo la mgodi, mradi unaotekelezwa na serikali kwa usimamizi wa TANESCO kwa gharama ya shilingi milioni 300.

Akizungumza kwa niaba ya wachimbaji hao, Mwenyekiti wa wachimbaji Madini ya dhahabu Mgodi wa Endagen, Abdul Amir Mwangu, amezitaja kero  zinazowakabili wachimbaji hao ni pamoja na ubovu wa miundombinu ya barabara,  inayopitika kwa msimu, ukosefu wa maji safi na salama, ukosefu wa huduma za mitandao ya simu, umeme, shule pamoja na zahanati.

Kwa unyenyekevu Mwenyekiti huyo, licha ya kumshukuru Mkuu huyo wa mkoa kwa kuwatembelea, ameiomba serikali kuwasaidia kutatua changamoto hizo ambazo zinakwamisha shughuli zao za kiuchumi, huku wachimbaji hao wakichangia pato la serikali kwa kulipa kodi zote muhimu.

"Mhe. Mkuu wa mkoa, sisi wachimbaji wadogo  tunakabiliwa na changamoto zetu hizo tano, ukiweza kutusaidia tutashukuru sana, mgodi una miaka 12 muda wote tunahangaikia kupata ufumbuzi wa changamoto hizi, kufika kwako tunaamini tumepona" Amesema

Baada ya Mkuu wa mkoa, kusikiliza kero hizo, ameziagiza Mamlaka za Maji RUWASA na TARURA kushughulikia changamoto hizo ndani ya mwezi mmoja kuona namna ya kuwawezesha wachimbaji hao kupata huduma hizo muhimu.

Amesema kuwa Rais wetu mama  Samia Suluhu Hassan anahitaji watalamu kutatua changamoto zinazowakabili wananchi na sio kuwaelezea michakato, tutakaa na watu wa TARURA kuona namna ya kutengeneza barabara lakini suala la shule na zahanati nalo serikali inalishughulikia.

"Suala la Umeme, TANESCO itakamilisha mradi huu  mwishoni mwezi Novemba, serikali imetoa milioni 300 za kukamilisha mradi huu, niwao doe hofu, umeme utawaka hapa na mtafanya kazi zenu kwa amani" Amefafanua Mhe. Mongella


Share To:

Post A Comment: