Na Munir Shemweta, WANMM KILIMANJARO

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Jerry Silaa ameagiza mmiliki wa mgahawa unaojulikana kama Fresh Restaurant uliopo Manispaa ya Moshi asisumbuliwe na badala yake asaidiwe ili aweze kulitumia eneo lake kulingana na matumizi anayohitaji.

Silaa ametoa kauli hiyo tarehe 5 Oktoba 2023 wakati akikagua maeneo mbalimbali ya Halmashauri ya Manispaa ya Moshi yanayolalamikiwa kujengwa ama kutumiwa kinyume na taratibu kwenye Halmashauri hiyo mkoani Kilimanjaro ikiwa ni juhudi zake za kuhakikisha uendelezaji miji unafuata taratibu.

Akiwa katika eneo hilo, Waziri Silaa alielezwa na Afisa Mipango Miji wa Manispaa ya Moshi  Richard  Emily kuwa, mwaka 1959 kiwanja kinachomilikiwa na mfanyabiashara huyo awali kilimilikishwa kwa Moshi Trade Company Limited na baadaye kubadilishwa umiliki ambapo kwa sasa kinamilikiwa na ndugu Baraka Hussein Mallya.

Kwa mujibu wa Afisa Mipango Miji huyo, mwaka 1987 yalifanyika marekebisho ya upimaji wa kiwanja hicho kwa kumegwa sehemu ya kiwanja yenye ukubwa wa mita za mraba 483 kama eneo la wazi.

‘’Eneo hili kwa mujibu wa michoro ya mipango miji ulioidhinishwa na Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi mwaka 1997, umetenga viwanja viwili vya matumizi ya makazi pekee’’. Alisema Emilly

Hata hivyo, alisema mwaka 2001 halmashauri ya Manispaa ya Moshi kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi waliandaa mpango wa uendelezaji eneo la mjini Kati ambapo sehemu ya kiwanja hicho lilipendekezwa kuwa eneo la wazi.

Kufuatia maelezo hayo, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Jerry Silaa ameshangazwa na namna halmashauri ya Manispaa ya Moshi inavyoshughulika na suala la umiliki wa kiwanja cha mfanyabiashara huyo.

‘’Ile Hati haikuwahi kuwa surrended, hamkutoa Hati mpya, mtu anamiliki eneo lake na analipia land rent lote sasa eneo la wazi mnalitoa wapi?’’ alihoji Waziri Silaa.

Ameitaka Halmashauri ya Manispaa ya Moshi kupitia watendaji wa sekta ya ardhi kuacha kumsumbua mfanyabiashara huyo kwa kuwa ana haki na anamiliki eneo lake kihalali ambapo amesema kama kuna uhitaji wa mabadiliko ya matumizi ya kiwanja basi wamsaidie na waondoe taharuki kwa wananchi.

Waziri Silaa amewahakikishia wananchi kuwa, akiwa kama Waziri wa Ardhi ataendelea kutenda haki bila kujali cheo, rangi wala sura kwa kuwa ameteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kuhudumia wananchi wote.

Amemtaka mmiliki wa kiwanja hicho kwenda kwa Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Kilimanjaro Rehema Jato ili asaidiwe  kama ni kubadilisha matumizi ya biashara na iwapo watu wa Mji wa  Moshi wataona inafaa basi asaidiwe katika hilo.

Katika ziara yake ya siku moja mkoani Kilimanjaro, Waziri Silaa mbali na kutembelea eneo la Mgahawa, alikagua pia eneo la Mawenzi Marathon Shabaha kata ya Mawenzi panapojengwa Kituo kidogo cha Mafuta pamoja na uwanja wa ndege Korongoni zinapojengwa nyumba tatu za makazi zisizokuwa na hati.

Waziri wa Ardhi alihitimisha ziara yake yenye lengo la kufuatilia utekelezaji wa Maamuzi ya Baraza la Mawaziri kuhusiana na Utatuzi wa Migogoro ya Matumizi ya Ardhi katika vijiji 975 kwa kuzungumza na watumishi wa sekta ya ardhi ambapo aliwataka watumishi hao kufanya kazi kwa weledi na kutoa huduma nzuri kwa wateja.

Share To:

Post A Comment: