1000274648


Na Immaculate Makilika - MAELEZO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema kuwa Serikali imeendelea kufanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya maji ili wananchi wa Mkoa wa Mtwara wanufaike na huduma hiyo.

Kauli hiyo ameitoa leo mkoani humo wakati akizungumza na wananchi katika  Uwanja wa Nangwanda Sijaona.

"Ujenzi wa Chujio la Maji utanufaisha asilimia 80 ya wakazi wa Mtwara na hii asilimia 20, Mhe. Waziri atangalia ni namna gani wananchi watapata maji ya kutosha wakati wote. Baada ya uwepo wa Chujio hili maji sasa ni safi na salama" amesema Rais Samia.

Naye, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema Serikali imeendelea kutekeleza miradi hiyo ya maji katika Mkoa wa Mtwara ili kutatua changamoto ya maji.

"Awali wananchi wa Mtwara walikuwa wakitumia maji yenye rangi na hivyo Serikali ilijenga chujio kwa gharama ya shilingi bilioni 3 na leo umeenda kulizindua" amesema Waziri Aweso.

Ameongeza "Mtwara ina mahitaji ya maji lita milioni 18, kwa sasa Mamlaka zetu zina uwezo wa kuzalisha lita milioni 14, upungufu ni lita milioni 4. Serikali imetoa bilioni 19 ili kutatua changamoto hiyo".

Pia, Waziri Aweso amebainisha kuwa ujenzi wa viwanda mkoani humo utahitaji maji ya uhakika na uelekeo wa Serikali ni kufanya maji ya Mto Ruvuma kufika Mtwara.

"Wananchi wa Mtwara niwaeleza kuwa Mhe. Rais Samia ameridhia na wadau watakwenda kutekeleza ndoto mliyoiomba kwa muda mrefu", amesisitiza Waziri Aweso 

Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ameendelea na ziara yake ya siku tatu Mkoani Mtwara ambapo jana amezungumza na wazee wa mkoa huo kwa lengo la kusikiliza kero zao na mapema leo ametembelea, kukagua na kuweka mawe ya msingi katika miradi ya Hospitali Rufaa ya Kanda Kusini - Mtwara, Chujio la Maji, Barabara ya Mtwara - Mnivata yenye urefu wa km 50, Bandari ya Mtwara na Uwanja wa Ndege.
Share To:

Post A Comment: