Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga ameweka historia kwa kuwasha umeme kwa mara ya kwanza katika Kijiji cha Ikindwa (Bukene) Wilayani Nzega mkoani Tabora, tangu kuanzishwa kwa kijiji hicho baada ya nchi kupata uhuru.

Kapinga amefanya tukio hilo, tarehe 25 Septemba 2023 katika Wilaya ya Nzega mkoani Tabora alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya Mradi wa Usambazaji wa Umeme Vijijini mzunguko wa tatu Awamu ya Pili katika wilaya hiyo kwa kuwasha umeme katika kijiji husika na kuzungumza na wananchi wa eneo hilo.

Akizungumzia Mradi huo, Mhe. Judith Kapinga amesema Serikali imetenga fedha nyingi kwa ajili ya kutekeleza mradi wa usambazaji umeme vijijini katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo vituo vya afya, taasisi za elimu, taasisi za dini, masoko, visima vya maji na mashambani.

“Niwatoe hofu kuwa Wananchi wote mtamfikiwa na umeme, kazi iliyombele yenu ni kusuka waya katika nyumba zenu, ili umeme utakapofika maeneo yenu kazi iwe ni kuwaunganisha tuu tena kwa gharama nafuu ya shilingi 27,000. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt Samia Suluhu Hassan ameshatoa maelekezo kuwa wananchi wote waunganishiwe umeme” alisema Kapinga.

Aidha ametoa siku saba kwa mkandarasi anaetekeleza mradi huo katika kijiji cha Ikindwa kuwalipa ujira wao vijana waliofanya kazi ya kuchimba mashimo, kusimika nguzo pamoja na kuvuta waya ambao mpaka sasa bado hawajalipwa fedha zao.

Alimueleza mkandarasi huyo kuwa jukumu la kusimamia malipo ya Wafanyakazi hao ni la kwake na si la Wakala wa Nishati Vijijini (REA) hata kama anaweka kampuni ya kumsaidia (Sub Contractor) katika kazi hiyo.

Sambamba na hilo aliwataka Wakandarasi wote kukamilisha na kukabidhi kazi waliyopewa ya kusambaza umeme vijijini ifikapo mwisho wa mwezi Desemba 2023 tena bila visingizo vya aina yoyote ili kumaliza kazi ya kusambaza umeme vijijini na kuhamia katika vitongoji.

Mhe. Kapinga amewagiza Wakandarasi kufanya kazi kwa weledi na uaminifu mkubwa na wafahamu kuwa jukumu la kuwaunganishia wananchi umeme ni la kwao, aidha hakuna mkataba utakaokamilika endapo mkandarasi hatamaliza kuwaunganishia umeme wananchi aliokabidhiwa.

Kwa upande wake Meneja Msimamizi wa Miradi kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi, Romanus Lwena amewataka wananchi kutumia umeme huo kwa shughuli za uzalishaji mali ili kujiletea maendeleo.

Mhandisi Lwena amewataka Wananchi kujitokeza kwa wingi kutumia fursa hiyo ya uwepo wa mkandarasi katika maeneo yao kwa kuandaa nyumba zao ili kuunganishiwa umeme na wasisubiri hadi pale Mkandarasi atapoondoka eneo la Mradi.

Baadhi ya Wananchi wa kijiji hicho wameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa kiasi kikubwa cha fedha kilichowezesha kupata huduma ya nishati ya umeme kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa kijiji hicho.

Wananchi hao wamemuahidi Naibu Waziri wa Nishati, kuwa watatekeleza ushauri wa kuandaa nyumba zao (Wiring); tayari kwa kuunganishiwa na huduma ua umeme pindi utakapofika katika maeneo yao.


Share To:

Post A Comment: