Na Mwandishi Wetu Mwanza

Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi, amesema mafanikio ya filamu ya “Tanzania; The Royal Tour” ambayo Rais Samia Suluhu Hassan alishiriki ili kuitangaza Tanzania yameendelea kuleta mafuriko ya mafanikio katika sekta hiyo.


“Tayari kwa takwimu za Benki Kuu ya Tanzania za Julai, 2022 hadi Julai, 2023 idadi ya watalii kutoka nje imefikia milioni 1.66 na mapato yamapaa hadi Dola za Marekani Bilioni 2.995 rekodi zote hizi hazijawahi kufikiwa wakati wowote katika historia ya nchi hii,” alisema Dkt. Abbasi akihutubia leo Septemba 8, 2023, kwenye mahafali ya 58 ya Chuo cha Taaluma ya Wanyamapori Pasiansi jijini Mwanza ambacho hufundisha askari wa wanyamapori na wataalamu wa kuongoza watalii.


Aliongeza kuwa uhifadhi ambao umechangiwa pia na wataalamu walioandaliwa na chuo hicho kwa miaka mingi nao umelipa ambapo leo Tanzania ina rekodi mbalimbali za Afrika na dunia ikiwemo kuwa miongoni mwa nchi za Afrika zenye tembo na faru wengi huku ikiongoza duniani kwa kuwa na simba na chui wengi.

Ametumia fursa hiyo kuwaomba wadau wa utalii na uhifadhi nchini kuwaajiri na kuwatumia vijana walioandaliwa vyema ikiwemo kutoka taasisi ya Pasiansi ili kuhakikisha utolewaji wa huduma bora katika sekta hiyo yenye ushindani mkubwa baina ya mataifa mbalimbali.

Share To:

OKULY BLOG

Post A Comment: