Kijana wa itifaki wa Chama Cha Mapinduzi CCM Wilaya ya Iramba, John Samwel akimvika skafu Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa baada ya kuwasili wilayani Iramba kwenye hafla ya  ya kumkabidhi Mkandarasi Henan Highway  Engineering Group Ltd ya nchini China mradi wa ujenzi wa barabara ya Singida, Sepuka, Ndago hadi Kizaga katika hafla iliyofanyika Septemba 9, 2023 wilayani humo mkoani Singida.

................................................

Na Dotto Mwaibale, Iramba

WAZIRI wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amewataka wananchi watakaopitiwa na mradi wa ujenzi wa barabara ya Sabasaba-Sepuka-Ndago-Kizaga mkoani Singida yenye  kilometa  77.6 kutojihusisha na hujuma yoyote ikiwamo  wizi wa vifaa ili ujenzi huo ukamilike kwa thamani iliyopangwa.

Bashungwa aliyasema hayo Septemba 9,2023 katika hafla ya kumkabidhi Mkandarasi Henan Highway  Engineering Group Ltd ya nchini China kuanza kazi ya ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami.

'' Serikali imetoa fedha nyingi za utekelezaji wa miradi mbalimbali kote nchini ikiwemo ya Mkoa wa Singida niwapongeze wananchi kwa ushirikiano mnaowapa wakandarasi hata hivyo nitoe tahadhari ya wizi wa mali na vifaa vitakavyotumika katika ujenzi naomba viongozi muwasisitize wananchi wanaozunguka maeneo ya mradi kuepukana na uhalifu wa aina yoyote wa vifaa hivyo badala yake wavilinde jambo litakalosaidia kulinda thamani halisi ya mradi huu na kukamilika kwa wakati na ubora unaokubalika,'' alisema Bashungwa.

Katika hatua nyingine Bashungwa amewataka Wakala  wa Barabara nchini (TANROADS), kuhakikisha wanamsimamia kikamilifu mkandarasi huyo na kukamilisha kazi hiyo kwa wakati uliopangwa na ubora.

" Tanroads nyie ndio wenye dhamana ya kusimamia ujenzi wa barabara hapa nchini  jipangeni vizuri ujenzi ukamilike ndani ya muda uliokusudiwa na kwa ubora na si vinginevyo", alisema Bashungwa.

Bashungwa alisema ujenzi wa barabara hiyo utagharimu Sh.Bilioni 88.583 bila kujumlisha kodi ya ongezeko la thamani VAT Sh.Bilioni 15.944 chini ya kampuni hiyo.

Bashungwa alitumia nafasi hiyo kumpongeza Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Mohammed Besta na watendaji wenzake pamoja na viongozi wote wa Mkoa wa Singida kwa kuandaa vizuri hafla hiyo na kueleza kuwa Singida imefungua njia na sasa ataanza ziara ya kwenda kuwakabidhi wakandarasi miradi iliyopo katika wilaya mbalimbali akiambatana na wabunge wa maeneo ilipo ambayo imekwisha tengewa fedha na Serikali.

Waziri wa Fedha Dk. Mwigulu Nchemba ambaye pia ni Mbunge wa Iramba Magharibi ambaye alikuwa mwenyeji wa makabidhiano hayo ya barabara hiyo pamoja na Mbunge wa Singida Magharibi, Elibariki Kingu, aliwataka watanzania kuwa wamoja hasa katika suala la kuinua uchumi wa nchi kazi ambayo Serikali ya Chama Cha Mapinduzi CCM imeianza kwa kushirikisha sekta binafsi katika uwekezaji wa uchumi.

'' Mimi kitaaluma ni mchumi hakuna nchi yoyote duniani ambayo inaweza kukuza uchumi wake pasipo kuwekeza kwenye sekta binafsi na katika jambo hili hatutarudi nyuma kwani litaongeza mapato ya nchi na kutuwezesha kutoa ajira nyingi, ikiwa ni pamoja na za wauguzi  ambao watakuwa wakifanya kazi kwenye vituo vya afya tulivyo vijenga nchi nzima,'' alisema Mwigulu.

Alisema kumekuwa na tofauti katika jambo hilo la uwekezaji hadi kufikia hatua ya kutaka kufarakana kati yao ambao wanaamini kupitia uwekezaji watapiga hatua na wenzao ambao hawautaki wakidai Serikali inaweza kufanyakazi hiyo peke yake.

Mwigulu alitumia nafasi hiyo kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za ujenzi wa barabara hiyo ambayo alikuwa ameanza kuiomba tangu alipoingia bungeni kwa mara ya kwanza ambayo inakwenda kuinua uchumi wa wananchi wa Wilaya za Ikungi, Iramba, Mkoa wa Singida na nchi kwa ujumla kutokana na kupata masoko ya mazao yao..

Mbunge wa Jimbo la Singida Magharibi, Elibariki Kingu licha ya kumshukuru Rais Samia kwa kutoa fedha za ujenzi wa barabara hiyo alitoa onyo kwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA, Freeman Mbowe aache kumsakama Rais Samia kwa kumteua Mohamed Mchengerwa kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI si kwa sababu ni mkwe wake bali inatokana na uchapakazi wake uliotukuka kabla hajawa waziri na baada ya kuwa Waziri  Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na , Wizara ya Maliasili na Utalii .

Akitoa taarifa fupi ya mradi huo, Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Mohammed Besta, alisema barabara hiyo inapita katika maeneo yenye uchumi wa kilimo, misitu, madini na rasilimali nyingi ambazo hazichangii kikamilifu kwenye pato la taifa kutokana na kutopitika kiurahisi.

‘’ Serikali inafanya jitihada za makusudi kuhakikisha maeneo yote ya kimkakati wa kiuchumi yanafikiwa kwa kuboresha barabara,’’ alisema Besta.

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba akitoa taarifa fupi ya maendeleo ya mkoa huo alisema una vijiji 441 kati ya vijiji hivyo vijiji 341 tayari vina umeme na vijiji 100 ambavyo havina wakandarasi wapo kazini.

‘’ Hapa Iramba wana vijiji 70 na vijiji ambavyo havina umeme ni vitano tu na hadi kufika mwaka kesho vijiji vyetu vyote vitakuwa na umeme,’’ alisema Serukamba.

Alisema mambo hayo yote yanafanyika kwa ufundi na ustadi wa Rais Samia Suluhu Hassan ambaye amefanya mambo mengi katika miradi ya maji, sekta ya elimu na mingine mingi ikiwemo minara ya simu na kilimo cha mazao yote alizeti, mpunga, mahindi, dengu, vitunguu, pamba na kueleza kuwa anaamini sasa kuwa Mkoa wa  Singida unakwenda kuwa kinara wa uzalishaji wa mafuta ya kula na mazao yote ya chakula na biashara yanayolimwa mkoani hapa..

Mkurugenzi wa kampuni hiyo ilipewa kazi ya kujenga barabara hiyo, Huang Lele alisema wamejipanga kukamilisha kazi hiyo kwa wakati uliopangwa na akaomba kupewa ushirikiano kwa kuzingatia kuwa China na Tanzania ni marafiki wa muda mrefu.

Katika mkutano huo Kamati ya maandalizi ya Kongamano la Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii Tanzania SMAUJATA ambalo litafanyika  Oktoba 7, 2023 ilitoa zawadi za fulana zenye nembo ya upingaji wa ukatili kwa mgeni rasmi wa hafla hiyo Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa na viongozi wengine mbalimbali waliokuwepo meza kuu zikiwa na ujumbe usemao Kataa Ukatili wewe ni Shujaa.

Mkutano huo ulinogeshwa na mandhari nzuri na majukwaa makubwa ya kisasa yaliyopangwa viti kwa ustadi wa hali ya juu na kupambwa na wafanyakazi wabobezi katika masuala ya uwekaji wa majukwaa na upambaji hapa nchini kwenye mikutano na matamasha na Kampuni ya Montage Ltd inayofanya kazi zake katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani yenye makao yake makuu jijini Dar es Salaam ambapo kwa mawasiliano nao unaweza kupiga simu namba 0754999010 au 0657185580. 

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, akimtambulisha kwa wananchi na kumkabidhi  ujenzi wa mradi huo Mkurugenzi wa kampuni hiyo ilipewa kazi ya kujenga barabara hiyo, Huang Lele.

Bashungwa akisisitiza jambo wakati akizungumza na wananchi wakati wa hafla hiyo.
Waziri wa Fedha, Dk.Mwigulu Nchemba akizungumza kwenye hafla hiyo.
Mbunge wa Singida Magharibi, Elibariki Kingu akizungumza kwenye hafla hiyo.
Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Dk.Kitila Mkumbo akizungumza.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba akitoa taarifa fupi ya maendeleo.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Singida, Martha Mlata akichangia jambo kwenye hafla hiyo wakati akitoa salam za chama.
Makamu Mwenyekiti wa Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii Tanzania SMAUJATA Mkoa wa Singida, Ambwene Kajula akimkabidhi fulana Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa yenye ujumbe usemao Kataa Ukatili wewe ni Shujaa.
Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Mohammed Besta, akiwa kwenye hafla hiyo.
Muonekano wa ukumbi huo uliopambwa na Kampuni ya  Montage Ltd.
Taswira ya hafla hiyo.
Vijana wa Hamasa wa CCM wakionesha umahiri wa kuruka wakati wa hafla hiyo.
Wakandarasi wa mradi huo wakiwa kwenye kampuni hiyo.
Hafla hiyo ikiendelea.
Mwenyekiti Mstaafu wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Singida, Seif Takaza akiwa kwenye hafla hiyo.
Wadau mbalimbali wakiwa kwenye hafla hiyo.
Wana CCM wakiwa kwenye hafla hiyo.
Viongozi hawa wakifurahia jambo wakati wa hafla hiyo. Kutoka kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Suleiman Mwenda, Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Thomas Apson na Mbunge wa Manyoni Mashariki, Dk. Pius Chaya.
Viongozi wa CCM wakiwa kwenye hafla hiyo.
Viongozi wakiwa kwenye hafla hiyo. Kutoka kulia ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida, Martha Mlata, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Singida, Yagi Kiaratu, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Innocent Msengi na Katibu wa CCM Mkoa wa Singida, Lucy Boniface.
Wananchi na makada wa CCM wakiwa kwenye hafla hiyo.
Msanii kutoka kikundi cha Sanaa cha  BMG cha Kata ya Ntwike, Joseph Sefu akionesha umahiri wa kucheza wakati akitoa burudani kwenye hafla hiyo.
Muonekano wa ukaaji mzuri baada ya viti kupangwa na wafanyakazi wa Kampuni ya Montage Ltd.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Wilaya ya Iramba, akionesha ufundi wa kusakata Rhumba wakati wa hafla hiyo ikiwa ni njia ya kuhamasisha watu.
Wajumbe wa kamati ya maandalizi ya kongamano la Smaujata litakalofanyika Oktoba 7, 2023 wakiwa kwenye hafla hiyo.
Hafla ikiendelea.
Msanii wa muziki wa kizazi kipya, Emanuly Zabron akipagawisha wakati wa hafla hiyo.


Viongozi wakiwa wamejipanga foleni wakati wakisubiri kumpokea mgeni rasmi Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa na mwenyeji wake Waziri wa Fedha, Dk.Mwigulu Nchemba.
Viongozi wa dini wakiwa kwenye hafla hiyo. Katikati ni Sheikh wa Mkoa wa Singida, Issa Nassoro.
Burdani zikiendelea kutolewa.
Wasanii wa kundi la Wajomba wakitoa burudani la kufa mtu.

Mkurugenzi Msaidizi wa Barabara, Wizara ya Ujenzi, Mhandisi Lightness Chobya akiwa kwenye hafla hiyo kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi.

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa akimkabidhi cheti cha heshima Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Suleiman Mwenda.
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa akimkabidhi cheti cha heshima Waziri wa Fedha, Dk.Mwigulu Nchemba. Vyeti hivyo pia walikabidhiwa viongozi wengine wa Halmashauri ya Wilaya.

Share To:

dotto mwaibale

Post A Comment: