Tanzania imepitishwa kuwa Mwenyeji wa mkutano mkubwa wa Nchi 25 wazalishaji wa zao la Kahawa Afrika(G-25).

Hayo yamesemwa leo katika Mkutano wa Pili wa nchi wazalishaji wa zao la Kahawa Afrika uliofanyika Jijini Kampala,Uganda na kufunguliwa na Rais wa Jamhuri ya Uganda Yoweri Kaguta Museveni.

Katika Azimio la Kampala(Kampala Declaration) imetamka bayana kwamba Mkutano wa Tatu wa Nchi wazalishaji wa Kahawa Afrika utafanyika Tanzania mwaka 2024 na hivyo azimio hilo kuitangaza Tanzania kama Mwenyeji wa mkutano huo mkubwa wa Kahawa Afrika.

Akizungumza katika Mkutano huo,Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango ameeleza bayana mikakati ya kukuza zao la

kahawa nchini Tanzania kutokana ongezeko la bajeti ya Wizara ya kilimo ambapo juhudi nyingi zimeelekezwa katika utafiti na uzalishaji wa miche bora ambayo husambazwa kwa wakulima kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa zao la kahawa ambapo uzalishaji wa zao la kahawa umeongezeka kutoka Tani 66,543 mwaka 2021/22 hadi kufikia Tani 82,491 kwa mwaka 2022/2023.

Aidha Makamu wa Rais Dkt. Mpango alitumia fursa hiyo kuwaalika nchi wazalishaji wa zao la kahawa katika mkutano wa tatu wa nchi 25 (3rd G-25 Africa Coffee Summit 2024) wazalishaji wa Kahawa Afrika utakaofanyika nchini Tanzania mwaka 2024.

Katika Ujumbe wake Makamu wa Rais ameongozana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mh. Balozi Mbarouk N. Mbarouk Naibu Waziri wa Kilimo Mh. Anthony P. Mavunde na wataalamu kutoka Bodi ya Kahawa Tanzania.

Share To:

Post A Comment: