Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) limeieleza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuwa linamiliki idadi ya Leseni 143 za uchimbaji madini ya aina mbalimbali zikiwemo leseni Mpya 3 za Madini ya Kimkakati ya Lithium, Graphite na Rare Earth Elements pamoja na kueleza utekelezaji wake.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Mkurugenzi wa Rasilimaliwatu na Utawala Deusdedith Magala Agosti 22, 2023 katika kikao cha Kamati jijini Dodoma, amesema kwamba, miongoni mwa leseni hizo, zipo zinazoendelezwa na Shirika, Kampuni Tanzu na ubia na kuongeza kuwa, Shirika linamiliki leseni ambazo zipo hatua mbalimbali za utafiti.
Akizungumzia leseni zilizo katika hatua ya utafiti ambazo zinahitaji uwekezaji, Magala amesema ni pamoja na zilizomo katika madini ya dhahabu, limestone, rubi, tin, nikeli, manganese, lithium, colbat, phosphate na copper.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Judith Kapinga ametoa ushauri kwa STAMICO kutafakari upya kuhusu mpango wake kwa kushirikiana na Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) na wawekezaji wa kuwekeza katika uzalishaji wa umeme wa Megawati 200 badala yake lifikirie kuzalisha kiwango kikubwa zaidi ili kukidhi mahitaji ya nishati ya umeme nchini na kuzingatia kuanzisha miradi yenye sura ya kitaifa.
Aidha, kwa upande wa wajumbe wa Kamati hiyo, mbali na kulipongeza Shirika hilo kutokana na juhudi kubwa iliyofanywa ya kuendeleza Sekta ya Madini ikiwemo kuwaendeleza wachimbaji wadogo, wameitaka STAMICO kuviongezea uwezo vituo hivyo ikiwemo kuongeza idadi yake kutokana na mahitaji ya watumiaji kwa lengo la kuongeza tija na kurahisisha shughuli za wachimbaji wadogo wa madini kutokana na matokeo yenye tija ambayo yamepatikana kupitia vituo hivyo.
Vituo vya mfano vilianzishwa kwa lengo la kutoa mafunzo ya uchimbaji na uchenjuaji bora na wa kisasa wa madini usioathiri mazingira na unaohamasisha matumizi ya teknolojia rahisi katika shughuli za uchimbaji mdogo. Hivi sasa kuna jumla ya vituo vitatu vya mfano vilivyoko katika maeneo ya Lwamgasa na Katente mkoani Geita na Itumbi wilayani Chunya.
Wakati akisoma hotuba yake Bungeni mwezi Aprili, 2023, Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko alisema katika kipindi cha Julai, 2022 hadi Machi, 2023 jumla ya gramu 30,475.72 za dhahabu zenye thamani ya shilingi bilioni 3.6 zilizalishwa kupitia vituo hivyo na kiasi cha shilingi milioni 279.6 zililipwa Serikalini.
Akizungumza katika kikao hicho, Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruwa amesema wizara imepokea ushauri wote uliotolewa na itaufanyia kazi ikiwemo kuisimamia Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) kufanyia utafiti leseni zinazomilikiwa na STAMICO.
STAMICO lilianzishwa mwaka 1972 likiwa na jukumu la kushiriki na kuendeleza rasilimali za madini nchini kwa niaba ya Serikali. Mwaka 2015, shirika lilifanyiwa maboresho kupitia Public Corporation (Establishment) (Amendment) Order iliyolenga kulifanya kuwa chombo madhubuti cha kuwekeza kimkakati katika Sekta ya Madini kupitia miradi mbalimballi ili kuongeza mchango wa Sekta ya Madini katika Pato la Taifa.
Miongoni mwa majukumu ya STAMICO ni kuwekeza kwenye miradi ya kimkakati ya utafutaji na uchimbaji madini; kuwekeza katika shughuli za uchenjuaji; uongezaji thamani madini na uuzaji madini; kutoa huduma za kibiashara za uchorongaji miamba na utafutaji wa madini;
Majukumu mengine ni kutoa huduma za ushauri wa kitaalam na kiufundi katika Sekta ya Madini zikihusisha ushauri wa kijiolojia, kihandisi, mazingira pamoja na uandaaji wa upembuzi yakinifu wa miradi ya uchimbaji au uongezaji thamani madini na kuratibu uendelezaji wa wachimbaji wadogo nchini kwa kutoaushauri wa kitaalam kwa wachimbaji hao.
Post A Comment: