Na Okuly Julius-Dodoma 


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya utumishi wa umma na Utawala bora , Mhe.George Simbachawene ,amesema Mamlaka ya Serikali Mtandao ni akili (Brain) ndani ya serikali kwa namna inavyotengeneza mifumo inayorahisisha utendaji kazi ndani ya Serikali na Taasisi zake.


Simbachawene ameyasema hayo Leo Agosti 23,2023 , Jijini Dodoma wakati akizindua mfumo wa kielektroni wa kukusanya , kuchakata na kutunza Kumbukumbu za kesi jinai utakaoimarisha utendaji kazi uliotengenezwa na Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS)


"Mamlaka ya Serikali Mtandao ni Brain ndani ya Serikali imerahisisha sana utendaji wa kazi serikalini na mfumo huu utasaidia kwa kiasi kikubwa kudhibiti makusanyo ya mapato ya Serikali,"amesema Simbachawene 


Simbachawene amesema kupitia mfumo huo mpaka sasa zaidi ya kesi za jinai 17,411 zimeshasajiliwa ambapo kati ya kesi hizo 7,361 zimeshafika mwisho na kutolewa hukumu huku kesi 10,050 zipo Katika hatua mbalimbali za maaumzi. 


"Kiukweli,haya ni mafanikio makubwa katika kuboresha utendaji kazi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS),lakini pia ni mfano wa kuigwa na taasisi nyingine za umma zinazohusika na utoaji wa huduma kwa umma,"amesema Simbachawene 


Amesema dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025 na Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2021/22 -2025/26), yote inatambua nafasi ya TEHAMA katika kufikia malengo ya Taifa na hivyo kusisitiza juu ya matumizi sahihi ya TEHAMA katika utekelezaji wa shughuli za Serikali na utoaji wa huduma kwa umma. 


Pamoja na mambo mengine, Sera ya Taifa ya TEHAMA ya Mwaka 2016, inasisitiza juu ya Serikali kutumia fursa zitokanazo na TEHAMA pamoja na matumizi sahihi na yenye tija ya Mifumo ya TEHAMA,katika kuboresha utendaji kazi wa Taasisi unaosaidia kutatua changamoto za kiutendaji, kudhibitimakusanyo ya mapato ya Serikali, kujenga na kuboresha uwezo,pamoja na kuimarisha mawasiliano miongoni mwa wadau wa Serikali Mtandao.


"Tumekusanyika hapa kwa lengo la kukabidhi Mfumo wa Kieletroni wa Usimamamizi wa Kesi,ambao unatambulikakama ‘Case Management Information System’(CMIS),pamojanaTovuti ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka

iliyosanifiwa na kujengwana Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA),kwa 

kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS)kwa kuzingatia sheria, kanuni, viwango na miongozo iliidhinishwa,"ameeleza Simbachawene 


Kwa Upande wake Naibu Waziri, Wizara ya Katiba na sheria Pauline Gekul amesema mfumo huo ni muhimu hasa kwa kuwa Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akisisitiza matumizi yake hali itakayo saidia kuimarisha na kurahisisha utoaji wa haki kwa wananchi.


Amesema katika kupitia dhamira hiyo huduma za serikali zitatolewa kidigitali na kumrahisishia mwananchi kupata huduma kwa haraka zaidi mahali walipo.


"Sote tunafahamu kuwa haki ni Suala muhimu sana na inapaswa kutolewa kwa wakati kwani haki iliyochelewa na sawa na haki iliyonyimwa hivyo Kupitia Mfumo wa TEHAMA tunataka kuhakikisha haki zote zinatolewa kwa wakati, "amesisitiza


Amesema, Sekta ya Sheria imejiwekea malengo thabiti katika kuboresha utendaji kazi wake kwa kutumia mifumo ya TEHAMA kupitia programu ya e-justice kuwezesha kupata taarifa za kesi mbalimbali zilizoshughulikiwa na hatua zilizofikia.


"Mfumo huu umeunganishwa Katika mfumo wa ubadilishanaji taarifa serikalini (GoVESB)na Hadi Sasa tayari unabadilishana taarifa za mifumo ya Jeshi la polisi pamoja na PCCB, "amefafanua.


Naye Mkurungezi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) Mhandisi Benedict Ndomba amesema malengo madhubuti ya mfumo huo ni kuhakikisha Taasisi zote za Umma zinaenda na wakati kwa kutumia TEHAMA.


Mhandisi Ndomba amesema kuwa mfumo huo umejengwa kwa lengo la kurahisisha upatikanaji wa taarifa

sahihi zinazohusu uendeshaji wa mashtaka na kusaidia katika uandaaji wa mipango ya ofisi na utoaji maamuzi mbalimbali pamoja na uandaaji wa taarifa zinazowasilishwa kwenye mamlaka nyingine.


Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) Sylvester Mwakitalu amesema kupitia Mfumo huo utamsaidia kuharakisha kesi zilizokuwa zinalundikana na kusababisha wananchi kusubiri kwa muda mrefu na kupoteza imani na Serikali.


"Tunaishukuru Mamlaka ya Serikali Mtandao kwa kutengeneza mfumo huu ambao kwa sasa naweza kufuatilia jinsi kesi zote zinavyoshughulikiwa na pale nitakapogundua kuwa kuna jalada limechelewa hapo hapo nauliza sababu za kuchelewa na linashughilikiwa kwa haraka,"amesema Mwakitalu 


Ikumbukwe kuwa, utekelezaji wa jitihada za Serikali Mtandao ni moja ya maeneo muhimu ya maboresho yaliyofanyika na yanayoendelea kutekelezwa katika Utumishi wa Umma, ambayo yamesaidia kuboresha utendaji kazi na utoaji wa huduma kwa Umma,hivyo, ujenzi wa mfumo huo ni muendelezo wa jitihada za Mamlaka za kuhakikisha Taasisi za Umma zinatumia vyema TEHAMA katika kuboresha utendaji kazi na utoaji wa huduma kwa Umma.
Share To:

OKULY BLOG

Post A Comment: