Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa nchi za Afrika wanachama wazalishaji wa zao la kahawa kuwekeza zaidi katika kupata vifaa na mashine za kisasa za uchakataji wa zao hilo ili kuongeza thamani ya kahawa kabla ya kuuzwa nje ya bara hilo.
Makamu wa Rais ametoa wito huo wakati akihutubia viongozi na wadau mbalimbali wa sekta ya kahawa Barani Afrika wakati wa Ufunguzi wa Mkutano wa Pili wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Nchi 25 za Afrika Wanachama Wazalishaji wa Zao la Kahawa unaofanyika Kampala nchini Uganda. Amesema ili kuinua sekta hiyo ni muhimu sekta binafsi kwa kushirikiana na serikali kuweka msisitizo katika kuongeza thamani ya zao hilo pamoja na kuwekeza katika vifungashio bora.
Aidha Makamu wa Rais amewasihi wakulima wa zao hilo kujikita katika kilimo bora na cha kisasa kwa kutumia teknolojia rafiki ili kuhakikisha sekta hiyo inakua na mchango mkubwa kwa wananchi na uhifadhi wa mazingira.
Pia Makamu wa Rais ametoa rai kwa Shirika la Kimataifa la Kahawa Afrika (IACO) kuharakisha maendeleo ya kituo cha ubora cha zao la kahawa nchini Tanzania kama ilivyokubaliwa hapo awali na kuahidi kwamba serikali ya Tanzania itatoa ushirikiano wote unaohitajika katika kufanikisha jambo hilo.
Makamu wa Rais ameeleza kwamba licha ya bei ya kahawa kuwa na mwenendo mzuri kwa kipindi kirefu bara la Afrika limeendelea kubaki nyuma kwa kuwa na asilimia 12 tu ya uzalishaji duniani huku mwelekeo katika ukanda huo ukiendelea kupungua kwa kasi. Amesema ni muhimu kutatua changamoto zilizopo na kuchukua hatua kuhakikisha fursa ya uzalishaji kahawa inatumika vema kwa kuzingatia kuongezeka kwa bei ya zao hilo duniani na uwepo wa soko la watu bilioni 1.4 lililopo Afrika.
Akitaja hatua mbalimbali zilizochukuliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuimarisha sekta ya kilimo ikiwemo kilimo cha kahawa, Makamu wa Rais amesema bajeti ya kilimo imeendelea kuongezeka katika kipindi cha miaka mitatu mfululizo ya kifedha, serikali inatoa ruzuku katika mbolea pamoja na kuongeza usambazaji bure wa mbegu za kiwango cha juu za zao la kahawa.
Ameongeza kwamba juhudi zingine ni pamoja na kuiwezesha benki ya maendeleo ya kilimo na kuhakikisha utoaji wa mikopo ya kilimo katika riba isiozidi asilimia tisa.
Aidha Makamu wa Rais amesema Tanzania imeendelea na jitihada za kuhakikisha wanawake na vijana wanashiriki katika mnyororo wa thamani katika uzalishaji wa zao la kahawa ikiwemo uanzishwaji wa Chama Cha Wakulima Wanawake wa Kahawa (TAWOCA), kuwawezesha vijana kimafunzo ili kuzalisha kahawa bora na kufanya biashara ya zao hilo.
Makamu wa Rais amesema kupitia hatua zilizochukuliwa, mafanikio mbalimbali yamepatikana ikiwemo kuongezeka kwa uzalishaji wa zao la kahawa kwa asilimia 19 kutoka tani elfu 66.5 mwaka 2018/2019 hadi tani elfu 82.5 mwaka 2022/2023.
Pia kuongezeka kwa fedha za kigeni kutokana na uuzwaji wa zao hilo kutoka dola za marekani milioni 123.2 mwaka 2018/2019 hadi dola milioni 235.6 mwaka 2022/2023 huku eneo la uzalishaji likiongezeka kutoka hekta 218,966 mwaka 2018/2019 hadi hekta 265,000 mwaka 2022/2023.
Mkutano wa Pili wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Nchi 25 za Afrika Wanachama Wazalishaji wa Zao la Kahawa umebeba kauli mbiu isemayo “Mageuzi katika sekta ya kahawa kwa kuongeza thamani”.
Mkutano huo umelenga kuendelea kusimamia ajenda ya kahawa katika orodha ya bidhaa za kimkakati chini ya umoja wa Afrika kupitia mpango wa Maendeleo ya Afrika (AU Agenda 2063).
Pia kuongeza thamani na matumizi ya ndani ya zao hilo, kupanua wigo wa biashara ya kahawa kupitia eneo huru la biashara Barani Afrika (AfCFTA) pamoja na kubadilisha uzoefu kuhusu za mabadiliko ya tabianchi na UVIKO19 katika sekta ya Kahawa.
Aidha Mkutano huo ni mwendelezo wa Mkutano wa kwanza uliofanyika Mei mwaka 2022 Jijini Nairobi nchini Kenya huku Mkutano wa Tatu ukitarajiwa kufanyika nchini Tanzania.
Kando ya mkutano huo Makamu wa Rais amekutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa Uganda Mheshimiwa Jessica Alupo.
Post A Comment: